1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yakanusha hitilafu katika vifaa vya maabara ya Tanzania

Daniel Gakuba
7 Mei 2020

Shirika la Afya Duniani, WHO leo hii limeyakataa madai ya rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kwamba kumekuwa na kasoro katika vifaa vya kupimia virusi vya corona katika maabara ya rufaa nchini humo.

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Rais wa Tanzania, John Pombe MagufuliPicha: DW/E. Boniphace

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa WHO kwa Afrika Matshidiso Moeti amesema shirika lake halikubaliani na kile alichokisema Rais John Pombe Magufuli.

Taarifa hiyo inatolewa baada ya Jumapili iliyopita rais huyo wa Tanzania kusema vifaa vya kupima vimekuwa na kasoro, na kubaini kupatikana kwa virusi vya corona katika papai na mbuzi.

Taarifa hiyo inafuatia ile ya awali ya Mkuu wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa na Kinga barani Afrika CDC, Dk. John Nkengasong ambaye alisema Tanzania inatumia vipimo vilivyotolewa na CDC ya Afrika kwa kushirikiana na wakfu wa mfanyabiashara wa kichina Jack Ma Foundation, ambavyo vimetimiza vigezo vya kimataifa.

Katika mkutano wake kwa njia ya simu na waandishi wa habari, mkuu huyo wa CDC  anasema kwa wanavyofahamu vifaa hivyo vinavyotumika Tanzania vinafanya kazi vyema kabisa na kwamba yapo mataifa mengine yanatumia vifaa kama hivyo.

Kwa upande wake msemaji wa serikali ya Tanzania amesema serikali imeunda timu ya wataalam, kuchunguza maabara hiyo iliyoendesha vipimo na itatoa matokeo yake baada ya uchuguzi kukamilika. Tanzania imethibitisha maambukizo 480 ya virusi vya corona na vifo 18.

                                                                                                                                                                         DPAE / 0123 / ECA /