1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yakemea kukosekana kwa usawa katika usambazaji wa chanjo

Daniel Gakuba
23 Desemba 2021

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni-WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema nchi tajiri haziwezi kushinda janga la corona kwa kuwapa chanjo ya ziada watu wao, zikishindwa kusambaza chanjo kwa usawa katika mataifa yote.

Genf WHO Direktor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHOPicha: DENIS BALIBOUSE/REUTERS

Mkurugenzi mkuu wa WHO ameyasema hayo katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, ambapo amekosoa vikali mipango iliyoshika kasi katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda, ya kuwaongezea chanjo watu wao, huku nchi maskini duniani zikiwa hazijamudu hada kutoa kinga ya mwanzo kwa raia wao.

Soma zaidi: Guterres ahimiza uratibu wa kimataifa katika vita dhidi ya COVID

Tedros alitambua ukweli kwamba chanjo dhidi ya covid-19 imenusuru maisha ya maelfu ya watu katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, akiongeza lakini kuwa kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa chanjo hiyo kunaweza kugharimu pia maisha ya watu wengi. Kukosekana huko kwa usawa, amesema Tedros, ni jambo lisiloeleweka.

Katika nchi zilizoendelea kiviwanda, watu wengi wanapata chanjo ya tatu kuimarisha mfumo wao wa kingaPicha: newscom/picture alliance

''Kusema kweli ni vigumu kuelewa kwamba mwaka mzima tangu chanjo ya kwanza ilipotolewa, wafanyakazi watatu kati ya wanne wa sekta ya afya barani Afrika bado hawajachanjwa,'' amesema Tedros na kulalamika kuwa wakati baadhi ya nchi hivi sasa zikiendesha kampeni ya kutoa chanjo ya ziada kwa watu wao, ni nusu tu ya nchi wanachama wa WHO ambazo zimeweza kuchanja angalau asilimia 40 ya watu wao, kwa sababu ya upotoshaji katika usambazaji wa chanjo duniani.

Asilimia 20 ya chanjo inatumiwa kuimarisha kinga katika nchi tajiri

Mkurugenzi wa WHO amesema kama chanjo ingesambazwa kwa usawa, kila nchi duniani ingekuwa imeweza kuchanja asilimia 40 ya watu wake kwa wakati huu.

Hali ni tofauti katika nchi zinazoendelea, ambako ni watu wachache wameweza kupata chanjo kamiliPicha: Evrard Ngendakumana/Xinhua/

Amenukuu takwimu zinazoonyesha kuwa asilimia 20 ya chanjo yote iliyopo hivi sasa inatumiwa kutoa chanjo ya tatu katika nchi tajiri, na kuongeza kuwa ripoti za hivi karibuni zinadhihirisha kuwa idadi kubwa ya wanaougua Covid-19 na kufika katika kiwango cha kulazwa hospitalini na hata kupoteza maisha, ni wale ambao hawajachanjwa.

Soma zaidi: Uingereza, Ufaransa kuchukua hatua mpya kukabiliana na Omicron

Wakati huo huo nchi nyingi za Ulaya zimeimarisha sheria za kuzuia kuenea kwa maambukizi ya kirusi aina ya Omicron, huku Ujerumani ikisema asilimia 20 ya maambukizi yote nchini yanatokana na kirusi hicho kinachosambaa kwa kasi.

Wimbi la tano lainyemelea Ujerumani

Mkuu wa taasisi wa Robert Koch inayoratibu mapambano dhidi ya Covid-19 Ujerumani, Lother Wieler amewatahadharisha wakaazi wa Ujerumani kuepuka mienendo ya kusaidia kusambaza maambukizi wakati wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, wakati Ujerumani ikionya juu ya uwezekano wa kupigwa na wimbi la tano la janga hilo.

Nalo shirika la kutengeneza dawa la kimarekani, pfizer limesema limeidhinisha dawa ya kwanza inayoweza kutumiwa na wagonjwa kujitibu Covid-19 wakiwa nyumbani kwao, tukio ambayo imesema ni hatua kubwa katika kupambana na janga la corona.

 

js/wd (AP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW