1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yakubali uchunguzi

20 Mei 2020

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limekubali kuanzisha uchunguzi kuhusu namna lilivyoushughulikia mzozo wa virusi vya corona, katika wakati ambapo China inaituhumu Washington kwa kukwepa wajibu wake.

Donald Trump - Schutzmaske
Picha: picture-alliance/S. Reynolds

China ilitoa shutuma hizo baada ya rais Donald Trump wa Marekani kutishia kujiengua kwenye shirika hilo. Hatua hiyo inakuja wakati maambukizi ya corona ulimwenguni yakikaribia milioni 5. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Gebreyuses alisema mapambano ya janga hilo ni lazima yawe ya kipaumbele, ingawa maradhi ya COVID-19 yanaendelea kusababisha vifo na kudhoofisha uchumi kote ulimwenguni. Rais Trump alilituhumu WHO kuwa ni kibaraka wa China na limeshindwa kufanya vya kutosha katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Idadi ya vifo imezidi kuongezeka katika baadhi ya maeneo, huku Uingereza ikifichua zaidi ya watu 41,000 wamefariki kutokana na maradhi ya COVID-19.

Siku ya Jumatatu, Trump alitishia kuondoa kwa muda ama moja kwa moja ufadhili kwenye shirika hilo, na China ilijibu kwa kumtuhumu Trump kujaribu kuichafua China na kuivuruga WHO kwa maslahi ya kisiasa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus amesema suala la kipaumbele kwa sasa ni mapambano dhidi ya coronaPicha: picture-alliance/Xinhua/WHO

Hata hivyo, profesa wa sheria ya afya ya ulimwengu kutoka chuo kikuu cha Georgetown Lawrence Gostin ameliambia shirika la habari la AP kwamba kitisho hicho cha Trump hakitatekelezeka kirahisi.

Alisema "Lakini pia hana mamlaka ya kufanya hivyo. Anahitaji bunge na hakuna namna kwamba bunge litamuunga mkono kuondoa ufadhili na kujiengua uanachama. Kusema kweli, sidhani ataweza kushinda ndani ya seneti hata ikulu." 

Soma Zaidi: Trump atishia kuiondoa Marekani kutoka WHO

Urusi pia ilikosoa kitisho hicho cha Trump. Umoja wa Ulaya inayoliunga mkono shirika hilo lilisema huu sio muda wa kunyoosheana vidole.

Nchini Brazil kumerekodiwa vifo 1,179 vya COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita. Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa idadi ya vifo ya siku moja kupindukia 1,000. Kulingana na wizara ya afya nchini humo, idadi jumla ya vifo imefikia 17,971. Maambukizi mapya katika muda kama huo yalifikia 17,408 na jumla ya watu 271,628 wameambukizwa.

Rais Jair Bolsonaro wa Brazil anakabiliwa na ukosoaji wa ndani na nje kuhusu namna anavyoshughulikia mzozo huo.Picha: picture-alliance/dpa/Palacio Planalto/M. Correa

Wataalamu wa afya ya umma wamesema kiwango cha juu kabisa kinatarajiwa kufikia mwanzoni mwa Juni, na kuongeza kuwa takwimu za serikali kwa kiasi kikubwa huenda hazitoi uhalisia wa vifo na maambukizi kwa kuwa Brazil inafanya vipimo vichache mno vya virusi vya corona. Siku ya Jumatatu, Brazil ilipanda hadi nafasi ya tatu, kutoka ya sita ulimwenguni kwa kuwa na maambukizi mengi, nyuma ya Marekani na Urusi.

Rais Trump amesema ataangazia kuliwekea taifa hilo zuio la kusafiri kufuatia hali hiyo.

Jijini New York, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Anthonio Guterres amependekeza baraza kuu ya umoja huo safari hii kufanyika kwa njia ya video. Baraza hilo ambalo hukusanya wanadiplomasia na maelfu ya maafisa mwezi Septemba, mwaka huu lingetimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake.

Na huko Mexico City, msajili wa vifo amesema kulikuwepo na vifo 4,577 ambavyo madaktari wanahisi huenda vilisababishwa na COVID-19, ikiwa ni mara tatu zaidi ya idadi inayotajwa na serikali. Serikali, imethibitisha vifo 1,332 katika mji huo ulioathirika zaidi tangu kuanza kwa janga hilo.

Mashirika: RTRE/APE/DW/AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW