1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yakutana kwa dharura kuhusiana na Ebola Uganda

Sylvia Mwehozi
14 Juni 2019

Jopo la wataalamu wa shirika la afya duniani WHO linakutana kwa dharura siku ya Ijumaa, ili kuamua iwapo liutangaze mripuko wa Ebola kuwa kitisho cha kimataifa baada ya ugonjwa huo kusambaa nchini Uganda. 

Ebola im Kongo
Picha: picture-alliance/dpa/A.-H.K. Maliro

Kamati ya dharura ya shirika hilo iliyoanzishwa mwaka 2005, imewahi kutangaza miripuko minne ya magonjwa kuwa kitisho cha kimataifa,  ikiwemo ugonjwa wa homa ya nguruwe, mripuko wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 hadi 2016 pamoja na virusi vya Zika.

Mgogoro wa sasa wa Ebola, ambao ulianzia mashariki mwa Congo mnamo mwezi Agosti umeshuhudia visa 2000 vikiorodheshwa na theluthi mbili kati yake vilikuwa vibaya sana. Jopo hilo la WHO, linalojulikana kama Kamati ya dharura ya kimataifa ya kanuni za afya limekutana mara mbili kuhusiana na mripuko wa Ebola nchini Congo. Katika mikutano yake hiyo miwili, haikuutangaza ugonjwa huo kuwa kitisho cha ulimwengu kwasababu haukuripotiwa katika nchi nyingine.

Lakini hali ilibadilika ghafla wiki hii baada ya watu wawili kuthibitishwa kufariki kwa Ebola magharibi mwa Uganda.

Wageni wanaowasili uwanja wa ndege wa Entebbe wakikaguliwa na afisa wa afyaPicha: picture-alliance/dpa/XinHua/J. Kiggundu

Mwanamke mmoja wa kikongo aliyeolewa na Mganda, pamoja na mama yake na watoto watatu na mlezi wao walisafiri hadi Congo kwa ajili ya kumuuguza baba yao aliyekuwa na maambukizi ya Ebola na baadae kufariki. Shirika la afya limesema wanafamilia 12 ambao walihudhuria mazishi nchini Congo waliwekwa katika karantini lakini 6 walitoroka na kurudi Uganda mnamo Juni 9.

Kwa mujibu wa WHO, mwanaume huyo anayedhaniwa kuwa ndiye aliyesababisha kusambaa kwa Ebola nchini Uganda alikuwa ni mchungaji na alikuwa hajulikani na maafisa wa afya kabla ya kufariki. Mkuu wa kamati ya dharura ya shirika la afya Dr. Mike Ryan amesema mchungaji huyo hakuwa kwenye orodha ya watu walio katika hatari ya kupata virusi vya Ebola. Kamati hiyo ya dharura inasema hakuna ushahidi kuwa Ebola imesambaa Uganda kwasababu hadi sasa mripuko huo umeripotiwa katika mkoa mmoja na kwamba mamlaka zinawafuatilia kwa karibu wanafamilia wote ambao wanashukiwa kuwa na maambukizi yake.

"Hakuna visa viingine ambavyo vimegunduliwa na kuna watu 27 ambao tumewabaini ndani ya familia ndani ya Uganda hadi sasa wako chini ya uangalizi," alisema Ryan.

Wakati huo huo, utafiiti mpya kutoka chuo kikuu cha Cambridge unaashiria kuwa nusu ya miripuko ya Ebola haikuweza kugundulika tangu virusi hivyo vilipojitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976. Utafiti huo uliochapishwa Alhamis unapendekeza juhudi zaidi kubaini dalili za mapema za mripuko wa Ebola. AP/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW