WHO yaonya kuhusu "kingamwili" ya virusi vya corona
26 Aprili 2020Wakati huo huo shirika la afya ulimwenguni WHO likionya dhidi ya "kuwapo kwa hati za uimara ya mwili" kwa wagonjwa wanaopona, kunakoonekana kuwa ni chombo cha mataifa kujitayarisha kufungua uchumi wao.
WHO inapinga, "hati" hizo kwasababu kupona kutokana na maambukizi ya virusi vya corona huenda kusimlinde mtu kutokana na maambukizi tena.
"Kwa sasa hakuna ushahidi kwamba watu ambao wamepona kutokana na maambukizi ya COVID-19 na wana chembe cha kingamwili wana uwezo wa kulinda dhidi ya kupata maambukizi mengine," shirika hilo la afya la umoja wa Mataifa limesema katika taarifa.
Wakati huo huo mamia ya mamilioni ya Waislamu duniani kote hawakuingia katika misikiti katika siku ya pili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuepuka kula pamoja kwa makundi katika familia wakati wa iftar kwasababu ya sera za kutokaa pamoja na kuweka umbali kati ya mtu na mtu.
Na Waaustralia na New Zeland wameadhimisha siku ya Anzac bila ya magwaride ya kawaida pamoja na sherehe za umma kuadhimisha wanajeshi waliofariki katika vita. Badala yake, chini ya utaratibu wa watu kukaa mbali mbali, watu walikaa nje ya nyumba zao usiku.
Hata wakati serikali kutoka Sri Lanka hadi Ubelgiji mpaka Marekani zikianza kuelekea katika kufungua nchi zao kwa kiasi fulani, janga la virusi vya COVID-19 bado limesababisha karibu nusu ya binadamu kuwa katika aina fulani ya kuzuiwa kutembea bila vizuwizi au kutakiwa kuwa katika majumba yao.
Maambukizi yamepanda
Jumla ya maambukizi duniani kote imepanda na kufikia watu milioni 2.86 na vifo vimefikia watu 200,000, ikiwa ni mara mbili tangu tarehe 10 mwezi Aprili, kwa mujibu wa idadi iliyokusanywa na shirika la habari la AFP.
Ulaya, eneo ambalo limeathirika mno , limerekodi vifo 122,171 vinavyotokana na virusi vya corona.
Idadi nchini Marekani imepanda kwa watu 2,494 katika kipindi cha masaa 24 na kufikia vifo 53,511. Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Marekani imepanda kwa karibu watu 46,000 hadi 936,293 tangu Ijumaa.
Nchini Italia , idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 imepanda hadi 26,384; Uhispania 22,902 , Ufaransa 22,614 na Uingereza 20,319.
Dunia inabaki ikisubiri wakati makampuni na serikali zinapiga mbio kutengeneza dawa na, hatimaye , kupata chanjo dhidi ya virusi hivyo, ambavyo vilizuka kwanza nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
WHO imeonya jana Jumamosi kuwa watu ambao wamethihirika kuwa wameambukizwa na wakapona kutokana na maambukizi hayo hawawezi kuwa na uhakika kwamba hawataambukizwa tena na virusi vya corona.
Onyo hilo limetolewa wakati baadhi ya nchi zikijitayarisha kufungua uchumi wake kwa matumaini kuwa wale waliambukizwa miili yao itakuwa na uwezo wa kujihami dhidi ya maambukizi mapya. Waziri mkuu wa Ufaransa Edouard Philippe kwa mfano siku ya Jumanne atawasilisha mkakati wa taifa wa kujitoa kutoka katika kufungwa nchi hiyo kutokana na virusi vya corona, ofisi yake imeliambia shirika la habari la nchi hiyo AFP.