1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

WHO yaonya kuhusu kuenea kwa magonjwa Gaza

17 Novemba 2023

Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuenea kwa magonjwa mbalimbali katika ukanda wa Gaza hasa wakati huu unapoanza msimu wa baridi.

Flüchtlingscamp NRWA
Mwanamke akitembea nje ya kambi ya wakimbizi wa Kipalestina huko Khan Younis,Gaza: 19.10.2023Picha: Belal Khaled/AA/picture alliance

Wasiwasi wa shirika hilo la Afya Ulimwenguni WHO kuhusu hatari ya kuenea kwa magonjwa huko Gaza, umetokana na kuendelea kwa mashambulizi ya jeshi la Israel ambayo yamevuruga mfumo wa afya na upatikanaji wa maji safi, na yamesababisha msongamano wa watu katika eneo moja.

Richard Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu amesema kufikia sasa, wameorodhesha zaidi visa 70,000 vya maambukizo ya magonjwa ya kupumua na zaidi ya visa 44,000 vya magonjwa ya kuharisha.

Soma pia:Gaza kutumbukia janga la kiafya - WHO 

Peeperkorn amesema hospitali ambazo zimeendelea kufanya kazi katika Ukanda wa Gaza zinakabiliwa na uhaba wa vitanda vinavyohitajika ili kuwahudumia wagonjwa na majeruhi wote katika eneo hilo.

Mwanamke wa Kipalestina akiwa amembeba mwanae wakielekea hospitali baada ya shambulio la Israel huko Khan Younis, Gaza: 15.11.2023Picha: Belal Khaled/AFP

Akizungumza kwa njia ya video na waandishi wa habari waliopo mjini Geneva naye akiwa huko Jerusalem, Peeperkorn amesema WHO inadhamiria kuanzisha hospitali za dharura katika Ukanda wa Gaza kufuatia uharibifu uliyosababishwa na mashambulizi ya Israel.

Mwakilishi huyo wa WHO amesisitiza kuwa kabla ya kuanza kwa vita, hospitali za Gaza zilikuwa na karibu vitanda 3,500 lakini leo hii zimesalia na vitanda 1,400 pekee, na kuongeza kuwa takriban wagonjwa 50 hadi 60 hulazimika kuondoka kila siku katika Ukanda wa Gaza ili kupewa huduma muhimu nchini Misri.

Soma pia: WHO kuanzisha hospitali katika Ukanda wa Gaza

Hayo yakiarifiwa, Jeshi la Israel limesema leo kuwa limewasilisha katika hospitali ya al-Shifa, zaidi ya lita 4,000 za maji na vyakula ambavyo tayari vimepikwa ikiwa ni sawa na milo 1,500.

Jeshi hilo ambalo pia limetangaza leo hii kuwa litaruhusu kila siku malori mawili ya mafuta kuingia Gaza, limesisitiza kwamba linatoa kipaumbelea kwa ustawi wa raia, wagonjwa na wafanyakazi wa hospitali.

Taarifa hii ya jeshi la Israel imetolewa wakati ambapo Umoja wa Mataifa ukitangaza kuwa haukuweza kusafirisha msaada hadi Gaza leo Ijumaa kutokana na uhaba wa mafuta na kukatika kwa mawasiliano.

Israel kupanua operesheni zake Gaza

Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi Picha: IDF/UPI/IMAGO

Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi amesema wanadhamiria kuendelea na kupanua operesheni yao ya kulitokomeza kabisa kundi la Hamas:

"Tunakaribia kabisa kuharibu mfumo wa kijeshi uliokuwepo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Kumesalia baadhi ya hatua na tunakaribia kufikia lengo hilo. Lakini tutalikamilisha. IDF itaendelea na operesheni zake huko Gaza na tutakuwa tukichukua udhibiti wa eneo baada ya jingine. Tutawaua makamanda na watendaji wa Hamas na kuharibu miundombinu yao."

Soma pia: Israel yaendesha operesheni ndani ya hospitali Gaza

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis atakutana wiki ijayo na ndugu na jamaa wa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas huko Gaza. Hayo ni kulingana na chanzo kilichozungumza na shirika la habari la Reuters.

Chanzo hicho kilichofahamika kama kiongozi mwandamizi wa Kanisa hilo Kadinali Pietro Parolin, kimeeleza kuwa Vatican inaamini kwamba kuachiliwa kwa mateka na kusitisha mapigano, jambo ambalo Israel imekuwa ikilitupilia mbali, ndio "masuala muhimu na ya msingi" ya kutatua mgogoro huo ambao kulingana na taarifa za kila upande, tayari umesababisha vifo vya waIsrael 1,200 na WaPalestina zaidi ya 11,500.

Kwa mara nyingine tena, maelfu ya watu wameandamana katika mataifa mbalimbali ya kiarabu ikiwa ni pamoja na Jordan, Lebanon, Qatar, ili kuwaunga mkono WaPalestina.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW