WHO yasema visa vipya vya COVID 19 vyaongezeka
16 Aprili 2021Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema katika mkutano uliyojikita juu ya Papua New Guinea na kanda ya Pasifiki Magharibi kwamba visa na vifo vinaendelea kupanda kwa viwango vya kutia wasiwasi.
Ameelezea wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea janga kubwa Papua New Guinea na kuongeza kuwa ni muhimu kwa taifa hilo kupokea chanjo zaidi za Covid-19 haraka iwezekanavyo.
soma zaidi: Wataalamu wa WHO kukutana kuijadili chanjo ya AstraZeneca
Hapo jana Mkuu wa shirika hilo la WHO barani Ulaya Dkt. Hans Kluge, amesema vifo vitokanavyo na virusi vya corona barani humo pekee vimepindukia milioni moja huku akisema hali bado ni mbaya mno wakati watu milioni 1.6 wakiambukizwa virusi hivyo kila wiki.
Kauli yake inanuwiwa kusisitiza kuwa ulaya ni lazima iendelee kuchukua hatua dhidi ya virusi vya corona na kuongeza kasi ya utoaji chanjo huku aina mpya ya kirusi ikiongeza maradufu idadi ya maambukizi katika mataifa mengine ya bara hilo.
Akizungumzia wasiwasi wa hivi karibuni juu ya chanjo tofauti. Dkt Hans Kluge amesema hatari ya kuganda kwa damu iko juu zaidi kwa watu wanaugua ugonjwa wa COVID 19 kuliko wale wanaopokea chanjo ya AstraZeneca