1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

WHO yatahadharisha kuhusu hatari ya 'kibayolojia' Sudan

25 Aprili 2023

Shirika la Afya Duniani WHO limesema wapiganaji katika taifa linalozongwa na vita Sudan, wamechukua udhibiti wa maabara ya umma yenye sampuli za maradhi kama polio na surua, hatua wanayosema ni hali ya "hatari sana”.

Konflikt im Sudan - Soldaten der paramilitärischen Rapid Support Forces
Picha: Hussein Malla/AP/dpa

Mwakilishi wa shirika la Afya Duniani  WHO nchini Sudan Nima Saeed Abid amesema wapiganaji waliwafukuza wataalam kutoka kwenye maabara hiyo, na kuchukua udhibiti wake na kuifanya kuwa kama kambi ya kijeshi.

Ametahadharisha kuwa kuna hatari kubwa ya kibayolojia inayoweza kutokea kutokana na uvamizi wa maabara hiyo kuu ya afya ya umma. Hasa ikizingatiwa ina sampuli ya maradhi hatari ikiwemo surua, ugonjwa wa kupooza na kipindupindu.

Soma pia: Milio ya risasi imerindima Sudan

Ameongeza kuwa kando na hatari za kemikali, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea hatari za kibayolojia kwa sababu majenereta hayafanyi kazi.

Abid ambaye hakueleza ni upande upi wa kivita umechukua udhibiti wa maabara hiyo, amesema alipokea simu kutoka kwa mkuu wa maabara ya kitaifa mjini Khartoum siku ya Jumatatu kuhusu hali hiyo.

Shirika la WHO limesema uvamizi na ukamataji wa maabara hiyo inazusha hali ya hatari ikizingatiwa inahifadhi sampuli za maradhi hatari.Picha: AFP/Getty Images

Mkurugenzi wa maabara ya kitaifa pia alitahadharisha kuhusu hatari ya kuharibika kwa akiba ya damu kutokana na ukosefu wa nishati kwenye maabara.

Soma pia: Burhan amani ya Sudan itapatikana kwa mazungumzo

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limesema limethibitisha mashambulizi 14 dhidi ya vituo vya afya wakati wa mapigano. Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu wanane na kuwajeruhi wawili.

Kulingana na takwimu za maafa zilizotolewa na wizara ya afya ya Sudan tangu machafuko yaanze, hadi Jumanne mchana watu 459 walikuwa wameuawa na 4,072 walikuwa wamejeruhiwa. Hata hivyo shirika la WHO limesema halijaweza kuhakiki kivyake kuhusu takwimu hizo.

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wahamiaji limesema linatarajia hadi watu 270,000 kutoka Sudan kukimbilia nchi jirani za Chad na Sudan Kusini.

Kamanda wa majeshi ya kitaifa ya Sudan Jenerali Abdel-Fattah BurhanPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Soma pia: Nchi za kigeni ziko mbioni kuwaokoa raia wao Sudan

Kulingana na Laura Lo Castro, mwakilishi wa shirika hilo nchini Chad, amesema takriban wahamiaji 20,000 wamewasili Chad tangu mapigano yalipoanza siku 10 zilizopita.

Wakati huo huo, mwenzake wa Sudan Kusini Marie-Helene Verney amewaambia waandishi wa habari kwamba shirika la UNHCR linatarajia hadi Wasudan 45,000 watakimbia nchi yao kuingia Sudan Kusini.

Mapigano nchini Sudan ni kati ya vikosi vitiifu kwa mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya vile vya naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza kikosi chenye nguvu kiitwacho Rapid Support Forces (RSF).

Je makubaliano ya kuweka mtutu chini yataheshimiwa Sudan?

This browser does not support the audio element.

Huku pande husika kwenye machafuko hayo zikiheshimu makubaliano ya kusitisha vita kwa saa 72 yaliyoafikiwa Jumatatu chini ya usimamizi wa Marekani, nchi za kigeni zimeimarisha juhudi zao za kuwaondoa raia wao walio kwenye taifa hilo la machafuko.

Vyanzo: AFPE, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW