1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yatangaza Ebola kuwa dharura ya kimataifa

Angela Mdungu
18 Julai 2019

Shirika la afya duniani WHO, limetangaza homa ya Ebola kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma. Tangazo hilo limetolewa baada ya taarifa ya kisa cha mgonjwa wa Ebola mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Genf Tedros Adhanom Ghebreyesus, Generealdirektor WHO | Ebola-Ausbruch Kongo
Picha: Reuters/D. Balibouse

Shirika la afya duniani WHO, limeutangaza  mlipuko wa homa ya Ebola nchini Congo kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma inayotia wasiwasi. Tangazo hilo limetolewa siku ya Jumatano baada ya taarifa ya kuwepo kwa kisa cha mgonjwa wa Ebola katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, siku chache zilizopita.

Timu ya wataalamu wa kamati ya kimataifa ya usimamizi wa afya, iliwahi kukataa mara tatu kulishauri shirika la afya la umoja wa mataifa kuutangaza mlipuko wa homa ya Ebola kuwa dharura ya kimataifa ingawa wataalamu wengine walisema janga hilo lina vigezo vyote vya kutangazwa. Zaidi ya watu 1600 wamekufa tangu mwezi Agosti mwaka uliopita, kutokana na ugonjwa huo ambao ni wa pili kwa kuua watu duniani. 

Tamko la ugonjwa kuwa dharura ya kimataifa mara nyingi husaidia kuleta hamasa na kushughulikiwa zaidi kimataifa na misaada kutolewa ingawa kuna wasiwasi kuwa zipo serikali zitakazoifunga mipaka yao kutokana na tangazo hilo. Tangazo hilo limetolewa siku chache baada ya kuthibitishwa kwa kisa kimoja cha ugonjwa wa ebola katika mji wa Goma, ambao ni njia panda iliyo Kaskazini Mashariki mwa Congo katika mpaka na Rwanda.

Kisa cha kwanza cha Ebola chathibitishwa Goma

This browser does not support the audio element.

 

Nchi zashauriwa kutofunga mipaka

Akitoa tangazo hilo mjini Geneva, mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wakati kukiwa na hatari ya kusambaa kwa Ebola, hatari kwa maeneo ya nje ya eneo hio bado ni ndogo. Ghebreyesus ameonya dharura hiyo isitumike kuwanyanyapaa ama kuwaadhibu watu wanaohitaji msaada.

Mhudumu wa afya akimpatia mtoto chanjo ya Ebola nchini DRCPicha: Reuters/O. Acland

Ghebreyesus amesisitiza kuwa shirika la afya duniani halishauri kuweka vizuizi katika safari ama biashara jambo ambalo badala ya kuzuia Ebola, linaweza kukwamisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo. Amesema kufunga mipaka kutasababisha janga kwa maisha na ustawi wa watu wanaovuka mipaka kila siku kwa ajili ya biashara, elimu ama kutembelea ndugu zao.

Tamko kama hili ni la tano katika historia duniani. Awali dharura za kiafya zilitangazwa mwaka 2014-2016 baada ya Ebola kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Afrika ya magharibi, na dharura nyingine ni ile ya homa ya Zika katika nchi za Amerika, homa ya nguruwe na ugonjwa wa polio.

Hata hivyo baada ya homa ya Ebola kutangazwa kuwa dharura ya kimataifa, waziri wa  wa afya wa Congo, Dr. Oly Ilunga ameonesha kusita kuupa ugonjwa huo hadhi ya kuwa wa dharura na kusema anakubali uamuzi wa kamati ya wataalamu lakini anatumaini kuwa uamuzi huo haukufanyika kutokana na shinikizo la makundi yanayotaka kujipatia fedha kwa ajili ya misaada. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW