1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yatoa idhini kwa Gavi na Unicef kununua chanjo ya Mpox

23 Agosti 2024

Shirika la Afya Duniani limeripoti kuwa washirika wake kama vile mashirika ya Gavi na Unicef, wanaweza kuanza kununua chanjo za homa ya nyani Mpox kabla ya kuidhinishwa kwa nia ya kupata chanjo barani Afrika.

DR Kongo | Mpox-
Mgonjwa wa Mpox nchini KongoPicha: Moses Sawasawa/AP/dpa/picture alliance

Shirika la Afya Duniani, WHO, limeripoti kuwa washirika wake kama vile mashirika ya Gavi na Unicef, wanaweza kuanza kununua chanjo za homa ya nyani Mpox, kabla ya kuidhinishwa kwa nia ya kupata chanjo barani Afrika huku kukiwa na ongezeko kubwa la ugonjwa huo barani Afrika. Wakati huohuo nchini Kenya, Wizara ya Afya nchini humo imeripoti kisa cha pili cha mgonjwa wa Mpox.

Kwa kawaida mashirika kama Gavi, ambayo husaidia nchi za kipato cha chini hununua chanjo za Mpox mara moja ambazo zinaweza kutumika baada ya Shirika la Afya duniani kutoa idhini ya kufanya hivyo.

Soma zaidi.Rais Tshisekedi wa DR Congo aidhinisha dola mil.10 kupambana na mlipuko wa mpox 

Chanjo mbili, zilizotengenezwa nchini Denmark na Japan tayari zimeidhinishwa na wadhibiti duniani kote, ikiwa ni pamoja na Marekani na Japan, na zimekuwa zikisambazwa kwa matumizi ya chanjo ya Mpox tangu 2022. 

Picha inayomuonyesha bintin mdogo ambaye ni mgonjwa wa mpox nchini Kongo Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Karibu watu milioni 1.2 wamepatiwa chanjo ya Mpox ya Bavarian Nordic nchini Marekani pekee.Shirika la afya duniani (WHO ) linatarajiwa kutoa leseni ya dharura kwa chanjo mwezi Septemba.

Huko Afrika Mashariki nchini Burundi visa 171 vya ugonjwa wa Mpox vimethibitiswa,  wizara ya afya ilisema hapo jana baada ya kutangazwa kwa kesi ya kwanza mwezi mmoja uliopita.

Soma zaidi. Wagonjwa 171 wa mpox wakutwa na mpox Burundi

Tukisalia kwenye ukanda huo wa Afrika Mashariki, Wizara ya afya nchini Kenya imethibitisha kisa cha pili cha ugonjwa  wa Mpox siku ya Ijumaa.

Hapo jana Shirika la Afya Duniani liliripoti mripuko wa virusi vya mpox vya Clade 2 kwa mara ya kwanza huko Ivory Coast kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ugonjwa huo katika nchi nyingi mnamo mwaka 2022.

Gabon yarekodi kisa cha kwanza cha Mpox

Kwingineko,  Wizara ya afya nchini Gabon imeripoti kisa chake cha kwanza cha mpox kwa mtu ambaye alikuwa amerejea kutoka safari ya Uganda nchi ambayo tayari imeathiriwa na janga hilo. 

Mtu mwenye ugonjwa wa Mpox Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Visa vya ugonjwa wa Mpox vimekuwa vikiongezeka Afrika Mashariki, lakini pia kwa sasa vimegunduliwa katika bara la Asia na Ulaya.

Tukirejea hapa barani Ulaya, Serikali ya Ujerumani kwa sasa inachunguza iwapo kuna dozi za chanjo ya mpox ambazo zinaweza kutolewa. Hayo yamesemwa na  wizara ya afya katika ripoti ya hali ya mwezi Agosti iliyoonekana na shirika la habari la  Reuters siku ya Alhamis.

Wizara ya Afya ya Ujerumani imeongeza kuwa hatua za mbalimbali za misaada ya kimataifa kuhusu namna ya kukabiliana na Mpox kama vile michango kutoka kwa Tume ya Ulaya inaendelea ingawa bado kunahitajika kufanyika kwa ufafanuzi zaidi ndani ya tume hiyo.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW