1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaunga mkono Michezo ya Olimpiki ya Tokyo

21 Julai 2021

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema Michezo hiyo ya Tokyo inapaswa kuendelea ili kuudhihirishia ulimwengu kile kinachowezekana kwa kuzingatia mipango na hatua sahihi. 

Japan Tokyo 2020 Olympia l IOC - WHO Ghebreyesus
Picha: Greg Martin/AFP

Katika hotuba yake leo kwenye kikao cha wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki mjini Tokyo, Tedros amesema ulimwengu unahitaji kwa sasa Michezo ya Olimpiki kama "sherehe za matumaini". Mbali na mashindano, mbali na medali, mbali na rekodi, michezo hii inayaleta mataifa ya ulimwengu pamoja katika kusherehekea, sherehe ya michezo, sherehe ya kusaidiana, sherehe ya mafanikio, sherehe ya urafiki na heshima, lakini mwishowe ni sherehe ya kitu muhimu zaidi, ya kitu ambacho ulimwengu wetu unahitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote, sherehe ya matumaini." Amesema Tedros

Michezo ya Tokyo inaanza Ijumaa Julai 23 wakati kukiwa na maswali kuhusu usalama wake, wakati maelfu ya wageni wakiwasili.

Tedros amekosoa kuwepo kwa utofauti kati ya nchi, akisema janga hilo lingemalizwa kama madola tajiri ya G20 yangeonyesha uongozi wa pamoja na kuwepo na usambazaji wa haki Zaidi wa chanjo. "Janga la COVID-19 limetuuliza maswali mengi kutuhusu na kuhusu ulimwengu wetu. Janga hili ni mtihani na ulimwengu unafeli. Zaidi ya watu milioni 4 wamekufa na zaidi wanaendelea kufa. Tayari mwaka huu idadi ya vifo ni zaidi ya maradufu ya idadi jumla ya mwaka jana." Ameongeza Mkuu huyo wa WHO. 

IOC imeahidi kupambana na COVID-19 kupitia michezoPicha: IOC/Xinhua/picture alliance

Michezo ya Olimpiki ambayo iliahirishwa mwaka jana kutokana na corona, itafanyika bila mashabiki viwanjani ili kupunguza kitisho cha afya.

Soma pia: Asilimia 80 ya Wajapan wapinga Michezo ya Olimpiki

Mpaka sasa kumekuwa na zaidi ya visa 67 vya maambukizi ya COVID-19 nchini Japan miongoni mwa waliopewa vibali vya kushiriki Mashindano hayo tangu Julai mosi, licha ya kuwepo hatua kali za kuingia nchini. Kufikia jana Jumanne, kulikuwa na visa 1,287 vya maambukizi mjini Tokyo. Tedros hata hivyo amesema Michezo hiyo haipaswi kuhukumiwa na idadi ya visa vya COVID-19 vinavyojitokeza kwa sababu haiwezekani kamwe kuondoa kitisho. Amesema jinsi maambukizi yatashughulikiwa ndicho kitu cha msingi.

Rais wa IOC Thomas Bach ameapa kuendelea kupambana na janga la corona kupitia michezo licha ya ukosoaji kuwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo inafanyika wakati kukiwa na ongezeko la maambukizi nchini Japan

Idadi ya visa vinavyohusishwa na tamasha hilo nchini Japan mwezi huu imefikia 79 leo, huku wanamichezo Zaidi wa kimataifa wakigunduliwa kuwa na maambukizi katika nchi zao na kushindwa kusafiri.

Watalaamu wa afya nchini humo wameonya kuwa Michezo ya Olimpiki itasambaza kwa kasi virusi kwa sababu inawaleta pamoja maelfu ya wanamichezo, maafisa, na wahudumu wakati huu ambapo kumetangazwa hali ya dharura mjini Tokyo.

AFP/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW