1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yautaka ulimwengu kupambana vikali na COVID-19

3 Agosti 2020

Shirika la Afya Ulimwenguni limeonya huenda kusipatikane suluhisho la haraka la janga la COVID-19 kwa maana ya chanjo mwafaka au dawa ya kuutibu ugonjwa huo

Schweiz | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: picture-alliance/KEYSTONE/M. Trezzini

Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limeonya leo kuwa huenda kusipatikane suluhisho la haraka la janga la COVID-19 kwa maana ya chanjo mwafaka au dawa ya kuutibu ugonjwa huo, na kuwa barabara ya kurejea katika hali ya kawaida itakuwa ndefu, wakati baadhi ya nchi zikihitajika kuupiitia upya mkakati wao. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanoma Ghebreyesus na mkuu wa WHO anayehusika na masuala ya dharura Mike Ryan wameyahimiza mataifa kutekeleza kikamilifu hatua za afya kama vile uvaaji barakoa, kutosogeleana, uoshaji mikono na upimaji wa virusi hivyo. 

Akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka makao makuu ya WHO mjini Geneva, Tedros amesema barakoa zinapaswa kuwa ishara ya mshikamano kote duniani. 

Corona: Juhudi za kutafuta chanjo ya COVID19 zapamba moto

03:23

This browser does not support the video element.

Timu ya Mwanzo ya WHO yakamilisha uchunguzi China

Mkuu huyo wa WHO pia amesema timu ya mwanzo ya uchunguzi imekamilisha ujumbe wake nchini China na kuweka mkakati wa utendaji kazi kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kutambua chanzo cha kirusi hicho. 

Tedros amesema, wakati virusi vya corona ndilo janga kubwa kabisa la dharura la kiafya kushuhudiwa tangu mwanzoni mwa karne ya 20, mapambano ya kimataifa ya kupata chanjo pia sio ya kawaida. 

Chanjo kadhaa sasa zipo katika hatua ya tatu ya majaribio ya binaadamu na kuna matumaini kuwa kupatikana aina kadhaa ya chanjo zinazofanya kazi ambazo zitawakinga watu dhidi ya maambukizi. Lakini Tedros amesema kwa sasa hakuna suluhisho la haraka na huenda lisiwepo katika siku za usoni. 

Naye mkuu wa WHO anayehusika na masuala ya dharura Mike Ryan amesema nchi zilizo na viwango vya juu vya maambukizi, zikiwemo Brazil na India, zinahitaji kujiandaa kwa mapambano makubwa. Kwa hiyo zitahitaji kutathmini upya mikakati yao ya kukabiliana na janga hili. 

Wakati huo huo, Iran imetangaza idadi kubwa kabisa ya maambukizi kuwahi kutokea kwa siku moja baada ya mwezi mmoja, ikionya kuwa nyingi ya mikoa yake imeathirika na wimbi la pili la ugonjwa huo. 

Maelfu ya watu waliandamana mjini Berlin mwishoni mwa wiki kupinga vizuizi vya kuzuia kusambaa kwa virusi vya coronaPicha: Getty Images/M. Hitij

Maandamano Ulaya kupinga vizuizi vya kuzuia corona

Licha ya kuzuka wimbi la pili, Ulaya imeshuhudia maandamano dhidi ya vizuizi vya virusi vya corona. Maelfu ya watu waliandamana mjini Berlin mwishoni mwa wiki wakiomba kile walichokiita kuwa ni “siku ya uhuru” kutokana na vikwazo vilivyowekwa. 

Janga hilo pia limeendelea kuvuruga sekta za usafiri, michezo, utamaduni na utalii, huku baadhi ya mashirika ya safari za ndege yakitangaza kuwafuta kazi wanyakazi wao wengi. 

Shirika kubwa kabisa la ndege Amerika Kusini, la LATAM, limesema litawafuta kazi wahudumu wake 2,700, wakati marubani wa Shirika la Ndege la Uingereza – British Airways wakiipiga kura kwa wingi kukubali mpango wa kupunguza mishahara yao kwa asilimia 20, huku nafasi za kazi 270 zikiwa tayari zimepotea. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW