1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yazilaumu kampuni za maziwa ya watoto kwa kupotosha

24 Februari 2022

Shirika la afya duniani WHO na lile la kuhudumia watoto UNCEF, yamezituhumu kampuni za maziwa kwa kuwalenga wanawake wajawazito na kina mama wadogo kwa kutumia mbinu za uuzaji zisizo za kimaadili.

Milchpulver Meji Japan Babymilch Radioaktivität
Picha: picture alliance/dpa

Ripoti mpya ya pamoja kutoka mashirika ya WHO na UNICEF inaeleza kwa kina kuhusu vitendo vya unyonyaji vilivyotmuiwa na sekta ya maziwa yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 55, kuhatarisha lishe ya watoto, na kukiuka maadili ya kimataifa.

Ripoti hiyo, inayoitwa: Namna Uuzaji wa Maziwa Unavyoathiri Maamuzi Yetu juu ya kuwalisha watoto wachanga, inatokana na mahojiano na wazazi, wanawake wajwazito na wafanyakazi wa afya katika mataifa nane.

Inafichua mikakati iliyoratibiwa na isiyo ya kimaadili ya uuzaji inayotumiwa na sekta ya maziwa ya Formula - ambayo sasa ina thamani ya dola bilioni 55 - ili kushawishi maamuzi ya wazazi ya kulisha watoto wachanga.

Wanawake wakiwapa watoto wao maziwa ya chupa wakati wanasubiri kupatiwa huduma katika hospitali ya Fuyang, mkoani Anhui nchini China, ambapo iliripotiwa kwamba watoto takribani 53,000 wa Kichina walidhurika baada ya kunywa maziwa ya formula yaliokuwa na uchafu, mwaka 2008.Picha: AP

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ujumbe unaopotosha na usiothibitishwa kisayansi unatumiwa kuwashawishi kina mama kuwapa watoto maziwa ya unga badala ya kuwanyonyesha. Utafiti huo unalinganisha uuzaji wa maziwa ya watoto na tumbaku au kamari, ambavyo vinaweka mbele mauzo kuliko afya ya mtoto na maendeleo.

Ripoti hiyo inasema kampuni zilianzisha au kujipenyeza kwenye makundi ya kina mama kwenye mitandao ya kijamii ili kupigia chapuo maziwa ya watoto, na kuwapa wafanyakazi wa afya taarifa zenye mashaka kwenye mikutano au vipeperushi, ambavyo baadae walivitoa kwa akina mama.

Taarifa hizo za uongo zilihusisha madai kwamba watoto wanalala kwa muda mrefu kwa kupewa maziwa ya Formula, kwamba maziwa ya mama yanapoteza ubora kadiri muda unavyokwenda, na kwamba baadhi ya bidhaa zinaweza kuzuwia mzio.

Dr Nigel Rollins, kutoka idara ya afya na uzazi na mtoto ya WHO, anasema kivutio kikubwa zaidi cha utafiti huo ilikuwa ni wingi wa ujumbe usio kikomo unaolekezwa kwa wanawake.

"Tunaona majukwaa ya mitandao ya kijamii yakitumika kwa wawakilishi wa masoko kufanya mawasiliano ya kibinafsi na wanawake mmoja mmoja," alisema Dk. Rollins.

WHO inahimiza wanawake kuwanyonyesha zaidi watoto wao kuliko kuwapa maziwa ya formula.Picha: AP

Nestle yaunga mkono udhibiti

Kampuni ya Nestle ya nchini Uswisi ni moja ya wazalishaji wakubwa zaidi duniani wa maziwa ya unga ya watoto.

Kampuni hiyo ilisema katika taarifa kwamba haitagazi maziwa ya watoto wa chini ya miezi 12 katika mataifa 163na kwamba, kufikia mwishoni mwa mwaka, itaacha kutangaza chakula cha watoto wenye umri wa hadi miezi sita kote duniani.

Nestle ilisema inaunga mkono uanzishwaji wa sheria kuhusu uuzaji wa chakula cha watoto katika mataifa yote.

Ni nchi 25 pekee ambazo zimetekeleza kwa mapana kanuni za maadili za mwaka 1981 kuhusu uuzaji wa chakula cha watoto, WHO iliripoti mwaka 2020.

Rollins anasema WHO haitazamii kupiga marufuku chakula cha watoto kutoka kwenye rafu za maduka, kwa sababu baadhi ya watoto wachanga wanahitaji chakula hiki.

Hasara za kutonyonyesha mtoto

01:30

This browser does not support the video element.

Lakini utafiti huo unahusu mbinu za uuzaji ambazo zinawadanganya akina mama ambao wanataka kunyonyesha, anasema.

Utafiti huo uliwahusisha wanawake wajawazito na kina mama wadogo 8,500 na wahudumu wa afya 300 katika nchi nane, ambazo ni Bangladesh, China, Uingereza, Mexico, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Vietnam.

Asilimia 51 ya waliohojiwa walisema walikuwa wamepokea matangazo kwenye mitandao ya kijamii, vyombo vya habari au katika kliniki.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW