1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Nchi tajiri acheni kujilimbikizia chanjo za COVID -19

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
19 Januari 2021

Shirika la afya duniani WHO limesema nchi tajiri zinajilimbikizia chanjo za COVID -19 bila ya kuzifikiria nchi masikini. Mkurugenzi mkuu wa WHO amesema mwenendo huo utaitumbukiza zaidi dunia kwenye janga la corona. 

Brasilien Corona-Pandemie | Impfstart | CoronaVac Sao Paulo
Picha: Nelson Almeida/AFP

Mkurugenzi huyo mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus pia ametahadharisha juu usambazaji wa kujipendelea wa chanjo za COVID-19 unaoweka pengo kati ya nchi tajiri na masikini, amesema mwenendo huo utazidisha ongezeko la ugonjwa huo.

Mkurugenzi huyo wa WHO ameongeza kusema kwamba kuongeza tu vizuizi wa ajili ya kuzuia kuongezeka maambukizi ya virusi vya corona pamoja na kwamba vinahitajika lakini hatua hizo zitawazidishia mateso wanadamu na uchumi utaendelea kuathirika duniani kote. Amezilaumu nchi tajiri kwa kununua na kujilimbikizia chanjo zote zilizopo kwa sasa.

Soma Zaidi:WHO: Mapambano ya COVID-19 yatakuwa magumu licha ya kuwepo chanjo

Zaidi ya dozi milioni 39 za chanjo sasa zimo mikononi mwa takriban nchi 49 tajiri. Ni dozi 25 tu zimepelekwa katika nchi moja peke yake yenye uchumi wa chini. Sio milioni 25, sio 25,000, bali ni dozi 25 tu, alisema mkurugenzi wa WHO wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wiki moja wa Bodi ya Utendaji ya shirika la afya duniani WHO hapo jana Jumatatu. Idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa COVID-19 ulimwenguni imepindukia milioni 93.8, na zaidi ya watu milioni 2.02 wamekufa, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: XinHua/dpa/picture alliance

Hapa nchini Ujerumani ijapokuwa hatua za karantini kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona zinaonekana kuleta mafanikio, Kansela Angela Merkel anataka kuongeza muda wa vizuizi hadi Februari 15 na pia kuweka sheria ya kuvaa barakoa zilizoidhinishwa kimatibabu kwenye vyombo vya usafiri wa umma na katika maduka. Kansela Merkel anatarajiwa kuyapendekeza hayo atakapokutana na wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani leo hii Jumanne kujadili hatua zaidi zinazofaa kuchukuliwa. Mkutano huo hapo awali ulipangiwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu.

Angalia:

Mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 hapa nchini Ujerumani wameelezea wasiwasi juu ya aina hiyo mpya ya virusi vya corona inayosambaa kwa kasi. Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema maambukizi mapya ya corona yameendelea kupungua katika siku za hivi karibuni na pia idadi ya wagonjwa waliolazwa kwenye wodi za kuwahudumia wagonjwa mahututi wanaougua COVID-19 imepungua kwa kiwango cha asilimia 10 hadi 15%.

Vyanzo:/RTRE/https://p.dw.com/p/3o6jq

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW