1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wickremesinghe aapishwa kuwa rais wa mpito

15 Julai 2022

Waziri Mkuu Sri Lanka Ranil Wickremesinghe leo ameapishwa kuwa rais wa mpito wa taifa hilo hadi bunge litakapomchagua mrithi wa Gotabaya Rajapaksa, Aliyejiuzulu kufuatia maandamano ya umma.

Sri Lanka | Vereidigung Interimspräsident Ranil Wickremesinghe
Picha: Sri Lankan President's Office/AP Photo/picture alliance

Aliyejiuzulu kufuatia maandamano ya umma kulalamikia kuporomoka kwa uchumi wa nchi na kumlazimu kuondoka madarakani.

Spika wa bunge Mahinda Yapa Abeywardana amesema Rajapaksa alijiuzulu rasmi kama rais jana Alhamisi na wabunge watakutana Jumamosi ili kuchagua kiongozi mpya. Spika huyo amesema kuwa kiongozi atakayechaguliwa na bunge, atahudumu kama rais kwa muda uliosalia wa Rajapaksa ambao unakamilika mwaka 2024.

Rajapaksa aitoka nchi

Picha: Amitha Thennakoon/AP Photo/picture alliance

Duru zinaarifu kuwa Rajapaksa aliwasilisha barua ya kujiuzulu muda mfupi baada ya kuwasili nchini Singapore siku moja baada ya kuikimbia nchi yake kufuatia shinikizo la maandamano ya umma.

Rajapaksa, mkewe na walinzi wawili waliwasili katika uwanja wa ndege wa Changi mjini Singapore City wakitokea visiwa vya Maldives ambako kiongozi huyo alikwenda baada ya kuitoroka Sri Lanka siku ya Jumatano.

Rais wa mpito Ranil Wickremesinghe amesema atafuata mchakato wa katiba na kuweka sheria na utulivu ndani ya nchi.

Wickremesinghe, amewataka wabunge kushirikiana ili kufikia muafaka wa kuanzisha serikali ya vyama vyote katika nchi hiyo iliyokumbwa na migogoro.

Mchakato wa kumchagua rais mpya

Spika wa bunge la Sri Lanka Mahinda Yapa AbeywardanaPicha: Rafiq Maqbool/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa Spika wa Bunge mchakato wa kumteua rais mpya utachukua siku saba. Na atakayechaguliwa na bunge kama rais anaweza kumteua waziri mkuu mpya, ambaye pia atapitia mchakato wa kuidhinishwa na bunge.

Spika Mahinda Yapa Abeywardana, amewaomba wananchi kudumisha amani

"Nawaomba wananchi waheshimiwa na wenye upendo kwa nchi hii, kuweka mazingira ya amani ili kutekeleza mchakato sahihi wa demokrasia ya bunge na kuwawezesha wabunge wote kushiriki katika mikutano na kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa uangalifu."

Sri Lanka imekosa pesa za kulipia uagizaji bidhaa za kimsingi na mahitaji kama vile chakula, mbolea, dawa na mafuta na kusababisha takriban watu mioni 22 wa taifa hilo la kisiwa kukata tamaa.

Kushuka kwa kasi kwa uchumi wake kunashangaza kwani kabla ya mgogoro huu, uchumi wa Sri Lanka ulikuwa umeimarika na tabaka la kati likiwa katika hali nzuri.

Awali serikali ya Sri Lanka ilikuwa imeanza majadiliano ya awali na Shirika la Fedha la Kimataifa kuhusu mkopo  wa ukozi ili kuwakwamua katika hali mbaya ya kiuchumi lakini majadiliano hayo yamesambaratishwa na machafuko ya hivi punde dhidi ya serikali.

Msemaji wa IMF Gerry Rice aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kuwa wafanyakazi wa hazina hiyo walikuwa bado wanawasiliana na maafisa wa serikali ya ngazi ya kiufundi na wanatarajia kuanza tena mazungumzo mara tu inapowezekana.

Sri Lanka imepokea msaada wa mabilioni ya dola kutoka taifa jirani, India, katika miezi ya hivi karibuni na pia ametafuta msaada kutoka China.

Vyanzo/Reuters, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW