1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Widodo aongoza katika uchaguzi wa Indonesia

17 Aprili 2019

Matokeo ya mwanzo yanaonyesha kuwa Rais wa Indonesia Joko Widodo ameshinda muhula wa pili wa miaka mitano kwa kumbwaga mpinzani wake wa saisa kali za kizalendo Prabowo Subianto

Wahlen in Indonesien   Joko Widodo
Picha: Reuters/E. Su

Matokeo ya kura zilizohesabiwa na mashirika matano huru ya uchunguzi unamuonyesha Widodo akiwa kileleni dhidi ya Subianto, jenerali wa jeshi wakati wa enzi ya utawala wa kidikteta wa jeshi la Suharto aliyeonya kuwa Indonesia itasambaratika kama haitakuwa chini ya uongozi wake wa kimabavu.

Mashirika hayo yanayonesha kuwa Widodo anaongoza kwa asilimia 54-56 ya kura. Akiwahutubia wafuasi wake saa chache baada ya vituo vya kura kufungwa, Widodo amesema anafahamu kuwa yuko kifua mbele katika uchaguzi huo na akatoa wito kwa taifa kuungana tena baada ya migawanyiko iliyoshuhudiwa wakati wa kampeni.

Subianto alishindwa na Widodo katika uchaguzi wa 2014Picha: picture-alliance/NurPhoto/D. Roszandi

Subianto, ambaye pia alishindwa na Widodo katika uchaguzi wa rais wa 2014, bado hajatoa tamko la kukiri kushindwa. Alisema uchunguzi wa mwanzo na wa haraka kutoka kwa timu yake ya kampeni unaonyesha kuwa ameshinda lakini akawaomba wafuasi wake kutozusha vurugu.

Timu yake ya kampeni inadai kutokea kwa dosari nyingi kwenye orodha ya wapiga kura, lakini wachambuzi wanasema madai hayo ni upuuzi na yanayolenga kuuhujumu uchaguzi.

Indonesia, taifa lenye idadi kubwa Zaidi ya watu wengi wao wakiwa ni waislamu, ni kitovu cha demokrasia Kusini Mashariki mwa Asia jirani na serikali za kimabavu na linatabiriwa kuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya kiuchumi duniani ifikapo 2030.

Muhula wa pili kwa Widodo, ambaye ni rais wa kwanza wa Indonesia kutoka nje ya tabaka la juu katika mji mkuu Jakarta, huenda ukauimarisha mchakato wa miongo miwili ya kidemokrasia nchini humo.

Zoezi hilo la uchaguzi lilikuwa changamoto kubwa huku kukiwa na wapiga kura milioni 193, Zaidi ya vituo 800,000 vya kupigia kura na watu milioni 17 waliohusika katika kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unaendeshwa kwa njia salama. Helikopta, boti, farasi vyote vilitumiwa kusambaza vifaa vya kupigia kura katika maeneo ya mbali na yasiyofikika kwa urahisi nchini humo.