1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Widodo: ASEAN haipaswi kuwa wakala wa dola yoyote

13 Novemba 2022

Rais wa Indonesia Joko Widodo ameapa kutoruhusu kanda ya Kusini Mashariki mwa Asia kuwa uwanja wa vita vipya baridi, mnamo wakati mvutano kati ya Marekani na China ukizidi kuongezeka.

 JOKOWI - ASEAN
Picha: Laily Rachev/Presidential Secretariat Press Bureau

Widodo amesema hayo mnamo wakati taifa lake limechukua uwenyekiti wa kupokezana wa jumuiya ya kiushirikiano wa nchi za kusini mashariki mwa Asia. Ameongeza kuwa taifa lake halitakuwa wakala wa dola yoyote yenye nguvu.

Widodo amesema jumuya hiyo yenye nchi 10 wanachama na iliyo na jumla ya takriban raia milioni 700, sharti iwe kanda yenye hadhi na ikuze sifa za ubinadamu na demokrasia, ambazo zimetiliwa doa kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar mwaka uliopita pamoja na wasiwasi kuhusu haki za binadamu nchini Cambodia.

Mkutano wa jumuiya ya ASEAN kuanza Ijumaa

"ASEAN sharti iwe kanda ya amani na iwe kitovu cha utulivu ulimwenguni, kila mara izingatie sheria ya kimataifa na isiwe wakala wa dola yoyote,” alisema. "ASEAN haipaswi kuruhusu hali ya sasa ya siasa za kiulimwengu kugeuka kuwa Vita Baridi katika kanda yetu.”

China imekuwa ikiimarisha ushawishi wake katika kanda ya Asia-Pasifiki na kusisitiza madai yake kuwa Taiwan inayojitawala kivyake kuwa ni sehemu yake. Marekani kwa upande wake imekuwa ikipinga hatua hizo, hali ambayo imezidisha mvutano.

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping watarajiwa kukutana Jumatatu.Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Mnamo wakati viongozi wa ASEAN wakikutana wikendi hii huko Phnom Penh, Marekani imekuwa ikiendelea na mazoezi yake ya kijeshi majini, katika bahari ya Ufilipino mashariki mwa Taiwan. Mazoezi hayo yanajumuisha washirika wa Marekani wa kundi lijulikanalo kama Quad. Kundi hilo linajumuisha Australia, India na Japan.

China yavurumusha makombora katika luteka za kijeshi karibu na Taiwan

Na mnamo Jumamosi, jeshi la China lilirusha ndege 36 za kivita karibu na Taiwan. Hatua hiyo imejiri kama sehemu ya juhudi ambazo zimeimarishwa na rais wa China Xi Jinping za kuitisha Taiwan. Mara kwa mara China imekuwa ikirusha ndege za kivita na zana nyingine baharini na karibu na Taiwan.

Rais wa Marekani Joe Biden aliyehudhuria mkutano wa kilele wa ASEAN, alisisitiza kwamba uhuru wa safari za baharini na angani Kusini na mashariki mwa China sharti uheshimiwe, na kwamba mizozo yote isuluhishwe kwa njia ya amani kulingana na sheria ya kimataifa. Hayo ni kulingana na Ikulu ya rais wa Marekani Whitehouse.

Biden amesema Marekani itashindana kikamilifu na China huku ikiwacha njia za mazungumzo wazi na ihakikishe ushindani wao haugeuki kuwa machafuko. White House imeongeza kuwa Biden pia alisisitiza umuhimu wa amani na utulivu wa Taiwan.

Jumuiya ya ASEAN yaadhimisha miaka 30 ya uhusiano wake

Rais wa Marekani Joe Biden (katikati) akikutana na rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol (kushoto) na Waziri Mkuu wa Japan (kulia) pembezoni mwa mkutano wa kilele wa jumuiya ya ASEAN, Novemba 13, 2022.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano wa ASEAN Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida pia alielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu majaribio ya China kutaka kubadilisha kwa nguvu hali iliyoko ya umiliki wa bahari za Mashariki na Kusini mwa China na vilevile shawishi za kiuchumi. Wizara ya mambo ya nje ya Japan imeeleza.

Wakati huo huo, viongozi wa Korea Kusini na Japan wamekubaliana kuendeleza juhudi za kusuluhisha mizozo tete ya kihistoria kati yao, mnamo wakati wakilenga kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na Marekani ili kuweza kudhibiti vitisho vya zana za nyuklia kutoka Korea Kaskazini.

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol na Fumio Kishida walikutana mara mbili na rais wa Marekani Joe Biden, pembezoni mwa mkutano wa ASEAN nchini Cambodia.

Kauli hizo zinajiri siku ´moja tu kabla ya mkutano unaotarajiwa kati ya Biden na Xi, katika mkutano wa kilele wa nchi katka kundi la G20 siku ya Jumatatu katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW