1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto na Samia kujadili kuhusu biashara na uwekezaji

4 Mei 2026

Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na William Ruto wa Kenya, wanashiriki jukwaa la pamoja la kujadili masuala ya biashara na uwekezaji kwa mataifa yao yanayotegemea sekta mbalimbali ikiwamo ukuzaji uchumi.

Tansania Daressalam 2026 | Präsident Ruto zu Staatsbesuch bei Präsidentin Hassan empfangen
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Kenya Dkt. William Samoei Ruto mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili.Picha: Tanzania State House

Viongozi hao wamekuwa na mazungumzo ya ana kwa ana ikulu jijini Dar es salaam kabla ya kujumuika na hadhira inayojumuisha viongozi wa kada mbalimbali kujadiliana masuala ya biashara na uwekezaji.

Jukwaa hilo ni uwanja unazingatiwa na pande zote mbili kwa ajili ya kusaka majawabu ya pamoja ya  namna bora ya kuvutia uwekezaji na kupunguza kile kinachotajwa kama vikwazo vya kikodi vinavyorudisha nyuma shughuli za kibiashara miongoni mwao.

Katika kipindi cha mwaka 2022 mawaziri wa uwekezaji wa pande zote mbili walitambua vikwazo 68 na kati yake 54 vilitafutiwa majawabu  kabla vingine vinne kuondolewa Oktoba mwaka jana.

Hadi wakati huu pande hizo mbili zinakabiliwa na vikwazo vipatavyo 10, na wataalamu wa mambo wanaamini kuwa kupitia kongamano hilo ambalo pia limewajumuisha wawekezaji wa sekta binafsi vinaweza kupatiwa majawabu.

Rais wa Kenya William Ruto yuko ziarani nchini Kenya anakotarajiwa kujadili masuala ya kibiashara na uwekezaji na mwenzake Samia Suluhu Hassan.Picha: Urs Flueeler/AFP

Paternus Niyegire ambaye ni mchambuzi wa siasa, uongozi na diplomasia anasema pande hizo zina nafasi kubwa ya kuendelea kufungua wigo wa kibiashara iwapo zitazidi kuonyesha nia ya kuondoa vikwazo vilivyosalia.

Anaamini kuwa, kuendelea kupunguzwa vikwazo hivyo kutoka 58 vilivyokuwa awali hadi kufikia 10, kunatoa matumaini juu ya uwezekano wa kumalizika mivutano ya kibiashara iliyoko.

Mazungumzo yananuiwa kutuliza mivutano ya kibiashara 

Licha ya maingiliano ya karibu yaliyopo kati ya Kenya na  Tanzania, mara kadhaa nchi hizo zimekuwa zikijikuta zikitumbukia katika mivutano ya kibiashara hali ambayo wengi wanaitazama imesababisha pia kuzorotesha ustawi wa kibiashara miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye nchi wanachama nane.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Kenya William Ruto Picha: Tanzania State House

Mapema akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo kabla ya kuwasili marais hao, Waziri wa nchi ofisi ya rais anayehusika na masuala ya mipango na uwekezaji Kitila Mkumbo alisema kwa namna yoyote ile mataifa hayo hayawezi kukwepana katika maingiliano yao.

Hivyo alisisitiza njia bora ya kuungana na kushirikiana katika kuziendeleza fursa zinazopatikana katika maeneo husika ili kuharakisha shabaha ya kukuza maendeleo. Aliitaja sekta binafsi kama uti wa mgongo wa pande hizo mbili kukimbia katika biashara.

"Kwa hiyo jukwaa hili ni muhimu kwa sababu linawaleta katika chumba kimoja watunga sera na sekta binafsi, hivyo ningependa kuwatia moyo kuzingatia mambo yanayotoa matokeo yenye uhaliisi”

Ndani yaJumuiya ya Afrika Masharikimataifa hayo mawili yanatazamwa kama mhimili wa kibiashara na kwamba tangu mwaka 2020 hadi 2024, nchi hizo zilichangia asilimia 40 ya biashara yote katika jumuiya hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW