Wimbi jipya la COVID-19 lazusha taharuki barani Ulaya
2 Novemba 2020Katika kile kinachoonekana kuwa ishara za kukata tamaa, waandamanaji kwenye miji kadhaa nchini Uhispania mwishoni mwa wiki walipambana na vikosi vya usalama kupinga kurejeshwa kwa marufuku ya shughuli za kawaida kujaribu kupambana na kitsho cha virusi vya corona.
Hivi sasa Uhispania inatekeleza amri ya kutotoka nje usiku na karibu majimbo yote ya nchi hiyo yameifunga mipaka ya ndani kuzuia safari za masafa marefu.
Serikali barani Ulaya zinahangaika kupunguza ongezeko la kutisha la maambukizi ya virusi vya corona ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 279,000 barani humo tangu vilipozuka nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
Nchini Uingereza, wengi wameelezea wasiwasi walio nao kuhusu hasara ya kiuchumi itakayopatikana katika muda wa wiki nne ambao shughuli zote za kawaida zitafungwa.
Huko Italia ambako kulishuhudiwa maandamano makubwa wiki iliyopita, serikali inatarajiwa kutengaza hatua mpya za vizuizi baadae hivi leo.
Duru zimearifu serikali inalenga kupiga marufuku safari baina ya majimbo nchini humo, kufunga maduka makubwa, kupunguza shughuli za biashara na kuzuia watu kutoka nje usiku.
Ujerumani nayo kuweka vizuizi vipya
Ujerumani hayo imeanza leo kutekeleza awamu mpya ya vizuizi ikiwa ni pamoja na marufuku ya mikusanyiko, kufungwa kwa kumbi za starehe na maduka yasiyo na bidhaa zinazohitajika kwa wingi pamoja na msisitizo kwa watu kuvaa barakoa.
Meneja wa mkahawa mmoja nchini Ujerumani aliyejitambulisha kama Christian Lehner amesema:
"Athari za kiuchumi wala hazipimiki tena. Mwaka huu wote unapaswa kusahaulika. Inafaa kuusahau mwaka huu mzima. Kabla ya marufuku ya kwanza, mwezi Februari, hakukuwa na cha kuingiza kwa sababu kila kitu kilishindana. Hata msimu wa kiangazi, ambako kwa baadhi ya wakati bustani zilijaa watu, ilikuwa ni sawa na tone kwenye bahari. Sasa tunaingiza sehemu tu ya kile tunachohitaji kuishi. Mwaka huu siyo wa kutengeneza tenapesa. Ni mwaka wa kujiokoa tu kiuchumi, kulinda ajira na kampuni."
Kwengineko waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex amesema kuanzia kesho Jumanne maduka makubwa yatapigwa mafuruku kuuza bidhaa ´zisizo muhimu´ kama ilivyokuwa kwa wauzaji wadogo waliolazimika kufunga maduka yao.
Mkuu wa WHO yuko Karantini
Wakati huo huo, mkuu wa shirika la Afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema anajiweka karantini baada ya kukutana na mtu ambaye sasa amebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, Tedros amesema bado yuko na afya njema bila dalili za COVID-19 lakini atasalia karantini kwa siku kadhaa zinazokuja kama taratibu za WHO zinavyoelekeza.
Tedros amesema ni muhimu kuzingatia miongozo ya wataalamu wa afya kwa lengo la kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona na kuikinga mifumo ya afya kutozidiwa na idadi ya wagonjwa.
Wiki iliyopita mkurugenzi huyo wa WHO aliwatolea wito viongozi wa dunia kuzingatia ushauri wa wataalamu katika wakati idadi ya maambukizi inapanda barani Ulaya na kwenye mataifa ya Amerika Kaskazini.