1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi jipya la ghasia lautikisa mji mkuu wa Libya-Tripoli

Daniel Gakuba
27 Agosti 2022

Wanamgambo wa serikali mbili zinazopingana nchini Libya wamepigana mjini Tripoli, na kuzusha wasiwasi wa kuibuka upya kwa vurugu wakati mkwamo wa kisiasa ukiendelea.

Libyen Armeekräfte in Tripoli
Picha: Yousef Murad/AP Photo/picture alliance

 

Watu wasiopungua 13 wameuawa katika ghasia hizo na wengine 95 wamejeruhiwa, ikiwa ni kwa mujibu wa duru za wizara ya afya nchini humo. Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa familia 64 zililazimika kuhamishwa kutoka eneo la mapigano.

Soma zaidi: Pande hasimu Libya zashindwa kuafikiana kuhusu uchaguzi

Miongoni mwa wahanga wa ghasia za Jumamosi ni Mustafa Baraka, mchekeshaji maarufu anayeitumia video za mitandani kudhihaki ubadhirifu na wanamgambo wenye silaha. Msemaji wa idara ya huduma za dharura, Malek Merset amesema Baraka aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani.

Merset amesema wafanyakazi wa msaada walikuwa wakifanya juhudi kuwaondoa raia waliojeruhiwa ambao wamenaswa katika mitaa iliyokumbwa na mapigano yaliyoanza usiku wa Ijumaa na kuendelea hadi Jumamosi.

Mapigano ya wanamgambo yameenea hadi mitaa ya makaazi ya raiaPicha: Arte/DW

Mashambulizi yailenga miundombinu ya kiraia

Tangazo la wizara ya afya limesema kuwa hospitali na vituo vya afya katika mji wa Tripoli vilishambuliwa, na magari ya kubeba wagonjwa yalikuwa yakitatizwa kufanya shughuli zao. ''Hilo linaweza kuwa uhalifu wa kivita,'' limesema tangazo hilo.

Baraza la mji wa Tripoli limewatwisha lawama wanasiasa juu ya kuzorota kwa hali ya mambo mjini humo, na limeiomba jumuiya ya kimataifa ''kuwalinda raia wa Libya.''

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waongeza muda wa ujumbe wake Libya kwa miezi mitatu

Machafuko haya mapya yamesababisha taharuki kwa wakaazi wa Tripoli. Picha za video zuimeonyesha majengo ya serikali, magari na makaazi ya watu yakiwa yameharibiwa kutokana na mapigano. Picha nyingine zimeonyesha wanamgambo wakiwa wanapelekwa katika mapigano, huku risasi zikirindima katika anga ya usiku ya mji mkuu.

Abdel Hamid Dbeibah, waziri mkuu wa serikali yenye makaazi mjini TripoliPicha: Mohammed El Shaikhy/AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa wahimiza kurejeshwa kwa utulivu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema silaha kubwa na za kati zimetumiwa ''kuishambulia kihelela mitaa yenye makaazi ya raia'' mjini Tripoli.

Ujumbe huo umetaka mapigano yasimamishwe mara moja, na pande zote zinazohusika ''ziepuke kutumia aina yoyote ya kauli za chuki na kuchochea vurugu.''

Soma zaidi: Uvunjaji sheria kiholela Libya kisiki kwa upatikanaji amani

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Libya, makabiliano haya ya umwagaji damu yamehusisha wanamgambo wa Brigedi ya Mapinduzi ya Tripoli inayoongozwa na Haitham Tajouri, dhidi ya kundi jingine la wanamgambo lenye mafungamano na Abdel-Ghani al-Kikli, mbabe wa kivita maarufu nchini Libya kama ''Gheniwa.''

Serikali ya Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah yenye makao yake mjini Tripoli imedai kuwa ghasia ziliripuka baada ya kundi moja la wanamgambo kulifyatulia jingine risasi.

Fathy Bashagha, waziri mkuu wa serikali nyingine ya Libya yenye makaazi mjini SirtePicha: Jihed Abidellaoui/REUTERS

Chanzo cha yote ni uwaniaji wa madaraka

Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa vurugu hizi ni sehemu ya mvutano wa madaraka kati ya Dbeibah na hasimu wake Fathy Bashagha ambaye pia amejitangaza kama waziri mkuu wa serikali nyingine yenye makao mjini Sirte.

Kila mmoja wao, Dbeibah na Bashagha anaungwa mkono na makundi ya wanamgambo, huku kima upande ukijaribu kuufurusha mwingine.

Soma zaidi: UN:Libya huenda ikawa na serikali mbili

Uhasama huu mpya umevunja hali ya utulivu ambayo imekuwa ikishuhudiwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta ilitumbukia katika mzozo baada ya vuguvugu la maandamano lililoungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO, ambamo kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gadhafi aliuawa.

-rtre, afpe, ape 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW