Wimbi jipya la wakimbizi kwenye mpaka wa Uturuki na Ugiriki
29 Februari 2020Polisi ya Ugiriki imetumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wakimbizi waliokusanyika kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Uturuki. Wakimbizi hao wamefika kwenye mpaka huo baada ya Uturuki kutangaza siku ya Alhamisi kuwa haitozuia tena wakimbizi walioko kwenye ardhi yake, ambao wanataka kwenda barani Ulaya.
Picha za video zilizoonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Skai cha nchini Ugiriki, zikichukuliwa kutoka upande wa Uturuki zimeonyesha polisi wa Ugiriki wa kupambana na ghasia wakitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya makundi ya wahamiaji, waliokuwa wakijibu kwa kuwarushia mawe na matusi.
Mpaka wa Ugiriki hautafunguliwa kwa wahamiaji
Ugiriki ambayo kwa muda mrefu imekuwa na mivutano na Uturuki, ilikuwa njia kuu iliyotumiwa na mamia ya maelfu ya wakimbizi walioingia barani Ulaya kati ya mwaka 2015 na 2016, mara hii inasisitiza kuwa haitaifungua mikono yake.
Msemaji wa serikali ya nchi hiyo Stelios Petsas amewaambia waandishi wa habari kuwa serikali hiyo 'itafanya chochote kinachowezekana kulinda mipaka ya nchi'.
Wimbi hili jipya la wakimbizi wanaojaribu kuingia Ugiriki limefuatia tangazo la Uturuki wiki hii, kwamba haitawawekea vizuizi wakimbizi wanaokimbia vita katika jimbo la Idlib nchini Syria, ambako wanajeshi 33 wa Uturuki waliuawa katika mapigano.
Hata hivyo, Petsas amesema mminiko huu wa wakimbizi 'hauhusiani kwa vyovyote vile na yanayojiri jimboni Idlib', na kuongeza kuwa katika muda wa saa 24 Ugiriki imewazuia wakimbizi 4,000 kuingia kwenye ardhi yake.
Hali ni tete mpakani
Mtu mmoja aliyeshuhudia hali hiyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wapatao 500 walikuwa wamepiga kambi katika eneo lililo katikati ya mipaka ya Ugiriki na Uturuki, na kwamba mamia wengine walikuwa wakisubiri upande wa mpaka wa Uturuki.
Mikanda ya video iliyoonwa na shirika la habari la Reuters pia ilionyesha baadhi ya wakimbizi wakiwavurumshia polisi vijinga vya moto usiku wa kuamkia Jumamosi.
Wakimbizi wengine wapatao 3,000 walikuwa wakingoja katika mji wa Kastanies ulio mpakani upande wa Uturuki, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa serikali ya Ugiriki.
Bila kutaja ushahidi wowote, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema wakimbizi takriban 18,000 tayari wamekwishaondoka Uturuki na sasa wako upande wa Ulaya.
Mazingira magumu kwa waandishi wa habari
Waandishi wa habari wanaofuatilia mzozo huu mpya wa wakimbizi kwenye mpaka wa Ugiriki na Uturuki wamezuiliwa umbali wa kilomita nzima nje ya mji wa Kastanies. Hata hivyo, baadhi waliweza kufika kwenye eneo jingine la mpaka ambako nchi hizo zinatenganishwa na mto.
Hapo walishuhudia kundi la wakimbizi kutoka Afghanistan, miongoni mwao wakiwemo watoto, likivuka mpaka na kutafuta hifadhi katika kanisa dogo lililo upande wa Ugiriki.
Viatu vyao vilikuwa vimejaa matope, yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo usiku wa Alhamis.
Mwaka 2015, wakimbizi wapatao milioni moja waliingia katika nchi za Ulaya wakitokea Uturuki, na kuungiza Umoja wa Ulaya katika mzozo mkubwa wa wahamiaji. Makubaliano yaliyosainiwa kati ya umoja huo na Uturuki mwaka 2016, yamekuwa yakisaidia kuwabakisha wakimbizi wengi upande wa Uturuki.
rtre,dpae