1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la 4 la corona laitikisa Ujerumani

11 Novemba 2021

Ujerumani imeripoti kiwango cha juu kabisa cha maambukizi ya virusi vya corona kwa siku moja, baada ya zaidi ya watu 50 elfu kuthibitika kuambukizwa virusi hivyo, ikiwa siku ya nne mfululizo ya kupanda kwa maambukizi.

BTW 2021 Themenbilder
Picha: Rupert Oberhäuser/imago images

Haya yanafanyika wakati ambapo wimbi la nne la maambukizi linaifagia nchi hiyo.

Watu 249 kati ya watu 100,000 Ujerumani wameambukizwa Virusi vya corona

Jumla ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani kwa sasa imefikia milioni 4.89 na watu 235 wamepoteza maisha hapo jana na kufanya jumla ya vifo kufikia 97,198. Taasisi ya Robert Koch inayohusika na afya ya umma Ujerumani imeripoti kwamba jana watu 50,196 waliambukizwa virusi vya corona.

Kiwango cha maambukizi ya virusi Ujerumani Picha: Rüdiger Wölk/imago images

Taasisi hiyo inasema katika kipindi cha wiki moja iliyopita kiwango cha maambukizi kimongezeka mno na sasa kati ya watu laki moja 249 wameambukizwa virusi hivyo.

Vyama vitatu vya kisiasa vilivyo kwenye mazungumzo ya kuunda serikali mpya vimekubaliana kutoongeza muda wa hali ya dharura ya kitaifa licha ya wimbi hili jipya la maambukizi. Badala yake, waliwasilisha rasimu ya sheria bungeni Jumatatu iliyopita, ili kutoa nafasi ya hatua za lazima kuchukuliwa kama kuvaa barakoa na kuweka umbali wa mtu hadi mtu katika sehemu za umma. Rasimu hiyo inataka hatua hizo ziendelee kuchukuliwa hadi mwezi Machi mwakani.

Huku hayo yakiarifiwa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameita mkutano wa dharura wa mawaziri viongozi wote wa majimbo ya Ujerumani baada ya ongezeko hilo la maambukizi ya virusi vya corona.

Msemaji wa serikali mjini Berlin Steffen Seibert amesema Merkel ambaye ana kaimu nafasi ya ukansela kwa sasa baada ya chama chake cha Kihafidhina kupoteza katika uchaguzi uliopita, anafanya mazungumzo ya mara kwa mara na mawaziri, serikali za majimbo na vyama vilivyo katika mazungumzo ya kuunda serikali, kuhusiana na janga la Covid-19.

Watu walio na zaidi ya miaka 65 sharti wapate dozi ya tatu ya chanjo Ufaransa

Lakini mawaziri viongozi wa majimbo 16 nchini Ujerumani hawajakubaliana ni lini watakapofanya mkutano huo na Kansela Merkel.

Raia akipokea chanjo ya Covid-19Picha: Jens Schlueter/Getty Images

Kwengineko waziri wa afya wa Ufaransa Olivier Veran amesema nchi hiyo iko mwanzoni mwa wimbi la tano la maambukizi ya virusi vya corona.

Ufaransa imeshuhudia ongezeko la maambukizi tangu katikati ya mwezi wa Oktoba na hapo Jumatano Rais Emmanuel Macron alitangaza kwamba kuanzia Disemba 15, watu walio na zaidi ya umri wa miaka 65 nchini Ufaransa, watahitaji dozi ya tatu ya chanjo la sivyo pasi zao za chanjo hazitokuwa na thamani.