1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Wimbi la joto Afrika Mashariki sasa laikumba Uganda

20 Machi 2024

Uganda imeanza kukumbwa na athari za wimbi la joto ambalo kwa sasa linashuhudiwa katika mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki hasa yale ambayo yako kwenye maeneo ya Ikweta.

Brasilien Hitzewelle und Trockenheit
Picha: BRUNO KELLY/REUTERS

Kiwango cha juu cha joto kisicho cha kawaida kimesababisha watu kuhisi kupoteza maji mengi mwilini pamoja na kuzuka kwa ugonjwa wa macho. Aidha, watu wamebadili ratiba zao ili kufanya kazi kabla ya athuhuri muda  ambapo jua limekuwa kali.

Athari za wimbi la joto ambalo kwa sasa linahisika sehemu mbalimbali za Uganda na mataifa jirani zimelazimu watu kuchukua tahadhari kuhusiana na afya zao. Kulingana na wataalamu, wimbi hilo limesababishwa na jua kuwaka zaidi kwenye maeneo ya ikweta katika msimu huu wa mwezi machi.

Lakini pia wataalamu wanaongezea kuwa uchafuzi wa hewa kwa kiwango cha juu cha hewa ukaa unatatiza upepo kupunguza mzunguko wa joto hewani na kwa hiyo kusababisha hali ya juu ya joto.

Uchafuzi wa mazingira umechangia

Miongoni mwa athari ambazo watu mbalimbali nchini Uganda wanahisi ni joto kali na kuonekana kuwa na kiu cha mfululizo hivyo kuwalazimu kunywa maji mengi.

Moshi kutoka kiwandaniPicha: blickwinkel/IMAGO

Dkt Peter Kibuuka ni msomi wa masuala ya hali ya hewa katika chuo kikuu cha Nkumba.

"Joto hili kali hasa maeneo ya mijini limezidishwa na uchafuzi wa hewa. Nawashauri watu kunywa maji na kula matunda badala ya chakula chenye viwango vya juu vya protini," alisema Dkt. Kibuuka.

Hali hii ya joto kali ni mbaya kaskazini mwa  Uganda na pia kwenye sehemu za miji kama Kampala.

Watu mbalimbali ambao huendesha shughuli zao hasa maeneo wazi yasiyo na vivuli wala paa wanaelezea kuwa wanakabiliwa na hali ngumu wakilalamika kuwa na kiu cha mfululizo.

Katika nchi jirani ya Sudan Kusini shule zimefungwa na wazazi kushauriwa kutowaruhusu watoto kuchezea kwenye jua.

 Unywaji maji waongezeka

Katika shule nchini Uganda walimu wameanza kupunguza vipindi vya watoto kushiriki michezo uwanjani na pia kuhakikisha kuwa wanakunywa maji ya kutosha na kupata vipindi vifupi vya mapumziko.

Mtu akiteka maji ya mferejiPicha: DW

"Tunachukua tahadhari mbalimbali ili watoto wasije wakapoteza maji mwilini lakini pia wasichoke upesi kutokana na joto kali," alisema Esther Otim, mwalimu wa shule ya msingi.

Hivi karibuni mripuko wa ugonjwa wa macho umeripotiwa katika magereza, shule na sehemu zenye msongamano wa watu.

Wataalamu wanasema kuwa mripuko huo ambapo hugeuka kuwa mekundu umesambaa kwa kasi kutokana na hali ya juu ya joto ambayo pia huandamana na pepo za mavumbi.

Kisa cha mbwa kumuua mtoto nyumbani kwao katika kitongoji jiani na mji wa kampala kimenasibishwa na hali hiyo baadhi ya wataalamu wakielezea kuwa wanyama hupoteza umakini wao na kufanya mambo yasiyofaa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW