1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaAsia

Wimbi la maambukizi ya Covid-19 bado laitikisa India

1 Mei 2021

India imeshuhudia siku nyingine mbaya ya janga la virusi vya corona kwa kuripoti kiwango cha maambukizi yaliyovunja rikodi siku ya Ijumaa wakati visa vya Covid-19 vipindukia milioni 150 kote duniani.

TABLEAU | Indien Coronavirus
Picha: Danish Siddiqui/REUTERS

Taifa hilo la Asia limerikodi visa vipya 385,000 vya Covid-19 ndani ya saa 24 zilizopita idadi ambayo haijawahi kufikiwa na taifa lolote duniani tangu kuanza kwa janga la corona.

India pia imearifu kuwa watu 3,500 wamekufa kutokana na kadhia hiyo ndani ya siku moja idadi ambayo waatalumu wengi wanashuku kuwa ndogo kwa sababu vifo vingi havirekodiwi.

Shehena ya msaada wa Covid-19 ikiwasili nchini India Picha: Prakash Singh/REUTERS

Nchi hiyo sasa inawakilisha asilimia 40 ya maambukizi yote ya Covid-19 duniani huku mfumo wake wa afya ukiwa umeelemewa vibaya na wanafamilia wanakosa maeneo ya kuchoma maiti kama ilivyo tamaduni za maziko kwa jamii kubwa ya wahindi.

Mataifa 40 yameahidi kutuma msaada wa dharura kwa India na tayari ndege ya kijeshi la Marekani iliyobeba shehena ya kwanza ya msaada unaojumuisha mashine za kusaidia kupumua na vifaa vingine vya matibabu iliwasili mjini New Delhi siku ya Ijumaa.

Jambo linalozidisha makali ya hali hiyo ni kushindwa kwa kampeni ya utoaji chanjo dhidi ya Covid-19 nchini India.

Hadi hivi sasa ni wafanyakazi wa huduma za afya na wale walio mstari wa mbele kwenye mapambano ya janga la corona pamoja na watu wenye magonjwa yanayotishia afya zao ndiyo wamekwishapatiwa chanjo.

Siku ya Jumamosi taifa hilo ndiyo linatarajia kuanza kuruhusu chanjo kuanza kutolewa kwa watu wazima na hiyo inaaminisha raia milioni 600 watahitaji kupatiwa huduma hiyo.

Kuna habari za kutia moyo huko Marekani 

Rais Joe Biden wa Marekani Picha: Andrew Harnik/AFP

Wakati hayo yakijiri nchini India, huko Marekani kuna habari njema baada ya taifa hilo kufanikiwa kuwachanja kikamilifu watu milioni 100.

Nchi hiyo imesambaza chanjo milioni 237 na hadi kufikia sasa asilimia 55 ya watu wazima tayari wamepatiwa angalau dozi moja ya chanjo.

Licha ya mafanikio hiyo, Washington imetangaza kuwa kuwa itaweka vizuizi kwa wasafiri kutoka India ikiwesema kiwango kikubwa cha maambukizi nchini humo kinaongeza uwezekano kwa virusi vya corona kujibadili maumbile.

Hadi siku ya Ijumaa janga la Covid-19 limekwishasababisha vifo vya watu milioni 3.2 kote duniani na linaendelea kuutikisa ulimwengu.

WHO yaidhinisha matumizi ya chanjo ya Moderna 

Juhudi za kutafuta matibabu zinaendelea. Siku ya Ijumaa Shirika la Afya duniani WHO lilitangaza kuwa chanjo dhidi ya virusi vya corona iliyotengenzwa na kampuni ya Moderna inaweza kutumika kwa dharura, na kuwa chanjo ya tano miongoni mwa zilizoidhinishwa na shirika hilo ili kutumika na amtaifa ulimwenguni.

Tangazo hilo limetolewa kupitia taarifa iliyotolewa na WHO ikisema lengo la hatua hiyo ni kuwezesha upatikanaji wa haraka wa dawa, chanjo na vifaa vya uchunguzi kukabiliana na dharura iliyopo

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO Mariangela Simao  alisema hapo kuwa kwa sasa ni muhimu kuwa aina nyingi za chanjo baada ya kujitokeza kwa changamoto ya usambazaji wake ikiwemo kutoka India, taifa ambalo linakabiliwa na wimbi kubwa la maambukizi ya Covid- 19.

Mbali ya Moderna WHO pia tayari imetoa ithibati kwa chanzo za Pfizer, AstraZeneca, Johnson & Johnson na nyingine iliyotengenezwa na taasisi moja ya India

     

     

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW