Wimbi la mgomo wa wafanyakazi lazidi kutapakaa Afrika Kusini
5 Oktoba 2012Wimbi la mgomo wa wafanyakazi nchini Afrika Kusini linaendelea kuchukua sura mpya kila uchao ambapo sasa Kampuni ya Toyota mjini Durban imesitisha shughuli zake kwa siku ya nne leo. Pia, chama cha wafanyakazi wa usafirishaji nacho kinawachochea wanachama wake wa reli na bandari kujiunga na wimbi hilo.
Zaidi ya madereva 20,000 wa magari makubwa wanatarajiwa nao kuitikia wito huo ambao unalenga kuizorotesha kabisa sekta ya usafirishaji nchini Afrika Kusini.
Mgomo huo wa madereva ulioitishwa hii leo umeathiri sekta ya usambazaji wa mafuta na ugavi kwa kiasi kikubwa. Na kama mgomo huo utajumuisha pia wafanyakazi wa reli na bandari utaathiri vikubwa biashara ya kupeleka nje bidhaa kama vile makaa ya mawe, platinum na dhahabu.
Migomo hii yaathiri uzalishaji viwandani na hivyo kuzorotesha uchumi wa taifa
Kampuni ya magari ya Toyota imesema imelazimika kufunga kiwanda chake cha magari cha nchini Afrika Kusini kwa siku nne kutokana na mgomo usio halali wa kudai nyongeza ya mshahara, wimbi lililoanzishwa na wafanyakazi wa migodini ambalo sasa linatapakaa nchi nzima.
Viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika kiwanda hicho kikubwa mjini Durban wamesema wafanyakazi watarejea kazini Ijumaa ya leo baada ya kuongezewa mshahara kwa asilimia 5.4.
Inasemekana madai hayo yanakuja, mwezi mmoja, baada ya kuona wafanyakazi wenzao wa Mgodi wa Platinum wa Marikana wakiongezwa mshahara baada ya kuendesha mgomo mkali.
Hata hivyo, Mbuso Ngubane wa Umoja wa Vyama vya wafanyakazi wa chuma nchini Afrika Kusini amesema mazingira na sababu za mgomo wa Toyota ni tofauti na mambo yanayoendelea katika migodi ya taifa hilo.
Ngubane ameongeza kusema kuwa hatua ya wafanyakazi wa Toyota kugoma inapeleka ujumbe chanya kwa wafanyakazi wa sekta zingine.
Chama Tawala kitahimili kishindo hiki?
Baada ya ghasia zilizodumu kwa miezi miwili sasa, takriban wafanyakazi 75,000 wa migodini ama asilimia 15 ya nguvu kazi katika sekta hiyo wamegoma kufanya kazi; hali inayozorotesha uchumi wa taifa hilo tajiri barani Afrika. Haya yanashuhudiwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa ndani wa chama tawala African National Congress (ANC).
Rais Jacob Zuma anapigiwa upatu kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 lakini kizaazaa hicho cha migomo kinaimarisha nguvu ya wale wanaodai kuwa Zuma sio mtu sahihi wa kuiongoza Afrika Kusini, nchi inayoshamiri upesi kiuchumi.
Katika hotuba yake kwa viongozi wa biashara hapo jana, Zuma alionekana kutotilia maanani migomo hiyo akiwataka vigogo hao kutokubali kuionyesha dunia kwamba taifa hilo liko katika mapigano.
Aidha, Zuma alisema na hapa namnukuu: "Tuna uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi iwapo tutafanya kazi pamoja kama Waafrika Kusini." Mwisho wa kumnukuu.
Jana hiyo hiyo, Mgodi wa chuma cha pua wa Kumba ambao ni moja kati ya wazalishaji 10 wakubwa zaidi duniani, ulisitisha uzalishaji katika kinu chake kikubwa cha Sishen baada ya wafanyakazi wake kuweka kizuizi katika lango la kuingilia mgodini.
Polisi mjini Rustenburg walionekana wakitumia gesi ya kutoa machozi jana na maji yanayowasha kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wakivurumisha mawe matairi yanayowaka moto. Msemaji wa polisi Thalani Ngubane amethibitisha taarifa hiyo na kuongeza kuwa hakuna aliyejeruhiwa wala kukamatwa.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul \ RTE
Mhariri: Mohammed Khelef