1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la nne la Covid-19 limefika kileleni barani Afrika-WHO

Daniel Gakuba
14 Januari 2022

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limesema kasi ya maambukizi ya virusi vya corona aina ya omicron inaanza kupungua barani Afrika, baada ya wiki kadhaa za kusambaa kwa haraka.

Südafrika Kapstadt | Impfung
Mhudumu wa Afya akiandaa dozi ya chanjo ya Covid-19Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Mkurugenzi wa shirika hilo anayehusika na hali ya dharura kiafya barani Afrika, Abdou Salam Gueye amesema Afrika inaondokana na kitisho cha wimbi la nne la covid-19. Aidha, afisa huyo amesema maambukizi yamekuwa yakipanda kwa kasi kwa wiki sita mfululizo lakini sasa kasi hiyo inashuka.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, wimbi hili la nne ndilo lililodumu kwa muda mfupi zaidi barani Afrika. Hata hivyo, ameonya kuwa viwango vya watu waliopokea chanjo Afrika vinabaki kuwa vya chini.

Nchi tajiri zatoa chanjo zinazokaribia kumaliza muda wake

Katika taarifa nyingine, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef limesema nchi masikini barani Afrika zinataabika kusambaza dozi za chanjo zilizotolewa kama msaada, kabla ya kumalizika muda wake.

John Nkengasong, Mkurugenzi wa kitengo cha Afrika cha kudhibiti magonjwaPicha: Mulugeta Ayene/AP/picture alliance

Katika taarifa hiyo kwa Bunge la Ulaya, Unicef imesema nchi tajiri zinazigawia nchi masikini chanjo ambazo muda wake wa mwisho kwa matumizi salama unakaribia. Limesema matatizo kwa nchi nyingi masikini yanazidishwa na ukosefu wa vifaa maalumu vya kuzitunza chanjo hizo.

Kwa mujibu wa Unicef, viwango vya chanjo ya msaada vimepanda, lakini utaratibu wa kuzisambaza kwa wahitaji bado unakabiliwa na changamoto.

Afrika yatafuta dawa ya kutibu Covid-19

Wakati huo huo, kitengo cha Afrika cha kudhibiti magonjwa, kimesema kinafanya juhudi kupata dawa aina ya Paxlovid, ambayo ina ufanisi wa asilimia 90 katika kuzuia maambukizi makali ya corona na kulazwa hospitalini.

Mkuu wa kitengo hicho John Nkengasong amesema wanafanya mazungumzo ya kina na kampuni ya kutengeneza dawa ya  Pfizer ambyo ndiyo mmiliki wa dawa ya Paxlovid, ili kuweza kuiagiza kwa ajili ya nchi za Afrika.

 

ape, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW