1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la nne la COVID latishia vizuizi vipya Ujerumani

17 Novemba 2021

Ujerumani hii leo imetangaza idadi ya juu kabisa ya maambukizi ya virusi vya corona wakati ikipambana na wimbi la nne la maambukizi lililoibuka tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba. 

Deutschland | Coronavirus Inzidenz
Picha: Rüdiger Wölk/imago images

Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ya Robert Koch  imesema leo kwamba imerekodi visa vipya 52,826 vya maambukizi katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita ambacho kulingana na taasisi hiyo ni cha juu kabisa tangu janga hilo lilipoanza mapema mwaka 2020 nchini Ujerumani.

Watu 294 zaidi wamefariki dunia kutokana na maradhi yanayohusiana na COVID katika kipindi kama hicho cha masaa 24 na kufanya idadi jumla sasa kufikia 98,274. Hata hivyo ongezeko hilo bado liko chini ikilinganishwa na ya mwezi Disemba mwaka jana. Kulingana na wataalamu hii inatokana na takribani theluthi mbili ya watu kuchanjwa.

Lakini pamoja na hayo, bado wanaonya kwamba idadi hiyo haitoshelezi ili kujihakikishia kwamba wamefanikiwa kuvidhibiti virusi hivyo. Wiki iliyopita mtaalamu wa maradhi yanayoletwa na virusi Christian Drosten alisema kutashuhudiwa idadi ya vifo ikifikia 100,000 iwapo idadi ya wanaopata chanjo haitaongezeka na hasa katika kipindi hiki cha baridi.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn anaonya kwamba ni lazima kuchukuliwe hatua zaidi kudhibiti maambukizi mapya.Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya shirikisho la Ujerumani wanatarajiwa kukutana kesho Alhamisi ujadiliana namna ya kupambana na wimbi hili la nne. Na hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa na watu watalazimika kuonyesha uthibitisho wa chanjo ama kuthibitisha kama wamepona maambukizi ya virusi hivyo iwapo watataka kuhudhuria matamasha na hata kuingia migahawani.

Baadhi ya maeneo pia yanataka uthibitisho wa chanjo ili kuruhusiwa kuingia kwenye masoko ambayo hufunguliwa wakati wa Christmas maarufu "Christmas Market". Hamburg ni miongoni mwa maeneo hayo. Masoko hayo huambatana na mapambo ya Christmas, shamrashamra za kila aina, vyakula na zaidi, mvinyo wa moto.

Nchini Ireland bar na klabu za usiku zitatakiwa kufungwa mapema ili kuendeleza kapeni ya utoaji wa chanjoPicha: Artur Widak/NurPhot/picture alliance

Kwenye maeneo mengine barani Ulaya huko Ireland, bar na klabu za usiku zitatakiwa kufungwa mapema, wakati ikizidi kuimarisha programu yake ya utoaji wa chanjo, katika jaribio la kukabili wimbi jipya la maambukizi. Serikali ya Ireland pia inawaomba watu kufanya kazi kutokea nyumbani. Vyumba vya huduma za wagonjwa mahututi tayari vimejaa pomoni. Waziri mkuu Micheal Martin amesema ni wazi kwamba taifa hilo linashuhudia wimbi jingine.

Huko Asia na Pasifiki, nako hali ni tete. Nchini China, serikali imeanza utetelezaji wa hatua mpya, na wageni wanaoingia Beijing sasa wanatakiwa kutoa uthibitisho wa kutokuwa na maambukizi. Idadi ya safari za ndege za ndani nayo imepunguzwa.

Nchini New Zealand, waziri mkuu Jacinda Arden amesema mji mkuu, Auckland utafunguliwa tena kuanzia Disemba 15 kwa wale waliopata dozi kamili ya chanjo na ambao vipimo vyao vinaonyesha hawana maambukizi. Auckland ilikuwa imefungwa kufuatia mlipuko wa kirusi aina ya Delta mwezi Agosti.

Soma Zaidi: Vifo vya COVID-19 vyapindukia milioni 5 duniani

Mashirika: DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW