Wimbi la pili la virusi vya corona laivamia Afrika
28 Desemba 2020Ripoti ifuatayo inaangazia ni mambo gani muhimu kwa sasa na kipi tulichojifunza kutokana na wimbi la mwanzo la virusi hivyo.
Iwe ni Afrika Kusini, Nigeria, Rwanda au Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, idadi ya visa vipya vya maambukizi ya virusi vya corona inaonesha kuongezeka katika sehemu nyingi za Afrika kwa kipindi cha wiki kadhaa.
Wimbi la pili la kusambaa kwa virusi hivyo ambalo limeshapiga muda mrefu katika sehemu nyingine za dunia, sasa linapiga pia katika bara la Afrika. Tangu kuzuka kwa virusi hivyo bara hilo limerikodi zaidi ya visa milioni 2.5 vya maambukizi huku idadi ya waliokufa ikiwa ni watu kiasi 59,000. Dokta Ado Mohammed, ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya afya wa kundi la nchi nane zinazoendelea zinazojiita D8 akizungumza na DW ameonesha wasiwasi wake kwa kusema wimbi la pili limewasili na watu wanapaswa kuwajibika na kuzingatia masharti.
Mamlaka za afya Afrika zimerekodi visa vipya vya wastani
''Wimbi la pili la Covid-19 limewasili Nigeria kama lilivyofanya pia kwenye nchi nyingine, kwa hivyo tunahitaji kuwajibika na kuzingatia hatua zilizopo na miongozo iliyowekwa. Lakini watu wamejisahau, shughuli zinafanyika kama kawaida, iwe ni mikutano, matamasha, sherehe za harusi. Watu wanasalimiana kwa kupeana mikono na unapokwenda misikitini na makanisani watu hata hawavai barakoa na wala hawakai kwa kuzingatia umbali wa kutokaribiana,'' alisema Dokta Ado Mohammed.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO mamlaka za afya katika nchi 47 barani Afrika zimerikodi kiwango cha wastani cha visa vipya 46,000 vya maambukizi kwa wiki tangu katikati ya mwezi Oktoba ikilinganishwa na visa 29,000 ambavyo viliripotiwa kwa wiki kati ya mwanzoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba.
Rwanda imetajwa kuripoti visa vingi vya maambukizi mapya mnamo mwezi Desemba tangu lilipozuka janga hilo, licha ya nchi hiyo kufunga vilabu vya pombe na vilabu vya usiku tangu mwezi Machi. Huko Kenya nako idadi ya maambukizi ilianza kuongezeka tena mwezi Septemba, na nchi hiyo sasa imeripoti visa vipya 20,000 vya maambukizi kwa wiki. Kukabiliana na hali hiyo serikali ikatangaza kuzifunga shule na kuongeza muda wa watu kutotoka nje. Hata hivyo mwanauchumi kutoka Nigeria Lawal Habib anasema kufunga shughuli za kimaisha Afrika sio mkakati wa muda mrefu wa kudhibiti ugonjwa huo.
''Hali tete ya uchumi wa Afrika haiwezi kuhimili wimbi la pili la kufunga kabisa shughuli zote za kiuchumi. Bado tunashuhudia athari za hatua ya mwanzo ya kufunga shughuli, tunashuhudia mfumko wa bei, bei za bidhaa na huduma kupanda, kutoweka na kuongezeka viwango vya umasikini na ukosefu wa ajira. Kufunga shughuli za kiuchumi tena hakutasaidia kitu bali kutaongeza tatizo la umasikini na ukosefu wa ajira,'' alisema Lawal Habib.
Afrika Kusini inakabiliwa na wimbi jipya la maambukizi pia
Afrika Kusini nayo pia inaonesha kuathirika na wimbi la pili la maambukizi. Kwa mujibu wa taarifa za Chuo Kikuu cha John Hopkins thuluthi moja ya visa vya maambukizi barani Afrika vinatokea Afrika Kusini. Nchi hiyo mwezi Julai kwa wiki kila siku iliripoti takriban visa 14,000 vipya vya maambukizi. Moja ya sababu zinazotajwa na wataalamu juu ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi nchini humo huenda ni kuzuka kwa aina mpya ya virusi hivyo vya corona ambavyo kwa muda fulani sasa vinaongezeka kwa kasi.
Hata hivyo ni kwa umbali gani virusi vya corona vimesambaa barani Afrika bado limebakia kuwa suala gumu kulitolea uamuzi. Ingawa kwa upande mwingine bara hilo pia linaweka matumaini katika chanjo mpya ambazo zimeidhinishwa katika baadhi ya nchi za dunia. Waziri wa Afya wa Nigeria, Osagie Ehanire ametangaza kwamba serikali ya nchi hiyo itapokea dozi milioni 20 ya chanjo ya Covid-19. Kenya nayo imeagiza dozi milioni 24 ya chanjo hiyo.
Japo nchi kama Afrika Kusini zinaweza kupokea shehena ya mwanzo ya chanjo hiyo kufikia mwezi Januari wataalamu wanahisi kwamba itachukua miezi kadhaa kabla ya chanjo hiyo kufikishwa kila nchi kwenye bara hilo. John Nkengasong mkuu wa shirika la kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afika CDC amesema kwamba chanjo hazitarajiwi barani Afrika hadi katikati ya mwaka 2021.