CHADEMA yashutumu vyombo vya dola kwa wimbi la utekaji
26 Oktoba 2025
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa rasmi kikidai kuwa vyombo vya dola nchini Tanzania vimekuwa na mchango mkubwa katika kile kinachoelezwa kuwa wimbi la utekaji wa watu 52 ndani ya siku 25, kuanzia tarehe 1 hadi 25 Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wengi wa waliotekwa ni viongozi wa chama hicho, wanachama wake, pamoja na raia wa kawaida, jambo linaloibua hofu kubwa kuhusu usalama na haki za binadamu nchini.
CHADEMA inasema matukio hayo yanaonyesha "uwepo wa mpango maalum unaoratibiwa,” ambapo watu wanaovaa kiraia au wanaojitambulisha kama maafisa wa usalama hutumia magari ya Land Cruiser bila namba za usajili kuwachukua watu kwa nguvu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya waliotekwa hawajulikani walipo hadi sasa, huku wachache waliopatikana wakiripotiwa kuwa na majeraha makubwa au hali mbaya ya kisaikolojia.
"Vyombo vya dola haviwezi kujisafisha kwa ukimya”
Katika orodha iliyotolewa na chama hicho, majina ya wahanga yanajumuisha walimu, viongozi wa tawi la vijana la chama hicho Bavicha, wanasiasa maarufu kama Humphrey Polepole, viongozi wa dini, na hata wanachama wa vyama vingine kama CCM.
Chama hicho kimeeleza kuwa baadhi ya matukio yalishuhudiwa wazi na wananchi, ambapo watekaji walijitambulisha kama askari kabla ya kuondoka na wahanga kuelekea kusikojulikana.
Msemaji wa chama hicho, Brenda Rupia, amesema:"Haiwezekani tukio la watu 52 kutekwa ndani ya mwezi mmoja bila vyombo vya dola kujua. Kama havijahusika, basi vinafahamu wahusika. Ukimya wao ni ushiriki wa moja kwa moja.”
'Vyombo vya dola vimepoteza uhalali wa kulinda raia'
Taarifa ya chama hicho pia inatoa mifano ya matukio yaliyohusisha Jeshi la Polisi, ikiwemo tukio la Wakili Dastan Mujaki ambaye alichukuliwa ofisini kwake na watu waliodai kuwa maafisa wa polisi, lakini baadaye hakuonekana tena katika vituo vilivyotajwa.
Vilevile, CHADEMA imehusisha tukio la Chief Kalumna, Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Bukoba, ambaye awali aliripotiwa kutekwa, kisha polisi kuthibitisha "wanamshikilia kwa uchunguzi maalum.”
Kwa mujibu wa CHADEMA, hali hii imezua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi na kuathiri imani kwa vyombo vya dola, ambavyo vinatakiwa kulinda raia bila kujali itikadi za kisiasa.
Ripoti hiyo pia inasema kuwa baadhi ya wahanga wamepotea wakiwa katika shughuli za kawaida — wengine wakitekwa kazini, wengine wakiwa nyumbani, na baadhi barabarani.
Tukio la Ayubu Juma, dereva bodaboda wa Ikungi, limeelezwa kama moja la kusikitisha zaidi baada ya mwili wake kupatikana porini siku tatu baada ya kutekwa.
Wataka serikali iunda tume huru kuchunguza
CHADEMA imetaka Tume Huru ya Uchunguzi iundwe mara moja kuchunguza matukio haya, ikisisitiza kuwa "ukimya wa serikali ni dalili ya kufumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu.”
Chama hicho pia kimetoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kufuatilia kwa karibu mwenendo wa usalama nchini Tanzania.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na usalama wamesema shutuma hizo ni nzito na zinahitaji majibu ya haraka kutoka serikalini.
Mmoja wa wachambuzi hao, aliyekataa kutajwa jina, alisema matukio haya yanaweza "kuashiria mgogoro wa ndani wa vyombo vya usalama” au "mwenendo wa kisiasa unaotumia hofu kama silaha ya kudhibiti fikra tofauti.”
Hadi sasa, serikali haijatoa tamko rasmi kuhusu shutuma hizo. Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa polisi waliotafutwa hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.
CHADEMA imesema itendelea kufuatilia na kutoa orodha kamili ya wahanga wote ikiwa serikali itaendelea kunyamaza.