1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la wakimbizi wa Afrika, nchini Israel.

Nyanza, Halima16 Aprili 2008

Hamed, ni mmoja wa wakimbizi wengi kutoka Afrika walioingia isivyo halali Israel kwa matumaini ya kupata kazi, lakini amejikuta bila ya shughuli yoyote ya kufanya.

Wakimbizi wa Darfur-Sudan, ni miongoni mwa wakimbizi kutoka Afrika, walio bahatika kupata ukazi wa muda Israel.Picha: picture-alliance/ dpa

Kijana huyo wa Kiafrika, ambaye amejipa jina la Hamed kwa kuhofia kuadhibiwa na serikali ya Israel, anaungana na wakimbizi wa Kiafrika elfu 7, waliowasili nchini humo tangu mwaka 2005.

Anasema alikimbia kutoka kwao Ivory Coast kwa sababu baba yake aliuawa, naye alihofia kuuawa na watu hao, hivyo na familia yake iligharamika kiasi cha dola elfu tatu kumuwezesha kuingia nchini Misri na halafu akalipa tena dola 800, kwa watu waliomvusha hadi katika mkoa wa Negev kusini mwa Israel mwishoni mwa mwezi wa pili, baada ya kusafiri kwa siku tatu kwa kutumia gari na kutembea kwa miguu kukatisha jangwa la sinai, huku akisikia milio ya risasi mpakani na fikira kuwa anaweza kuuawa.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, walinzi wa mpakani nchini Misri wameshaua wakimbizi 10 wa Kiafrika wanaojaribu kuingia Israel wakiwemo Wa Ivory Coast wawili.

Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limeitaka Misri kuchunguza mauaji hayo.

Shirika hilo limedai serikali ya Israel imekuwa ikiishinikiza Misri kupunguza idadi ya Waafrika wanaoingia nchini humo isivyo halali, matokeo ambayo mwanaharakati wa haki za binadamu Ilan Lonai anasema ni matumizi yasiyolingana ya nguvu yanayotumiwa na walinzi wa mpakani wa Misri.

Lonai ameeleza kuwa Israel haipaswi kuitumia Misri kuzuia watu wanaohitaji ulinzi kuingia nchini humo.

Steven Wolfdson kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR mjini Tel Aviv, anasema kiasi cha wakimbizi elfu 2 na mia mbili wamewasili nchini Israel katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hali inayofanya kuwa tatizo kubwa.

Wengi ya watu hao wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi ni kutoka Eritrea na Sudan.

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeripoti kuwa maelfu ya vijana wa kiume wameikimbia Eritrea kuepuka kuandikishwa kulitumikia jeshi.

Nchini Sudan kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binadamu, watu milioni 2.5 wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takriban miaka 22 na wengine milioni 2.5 wameyakimbia makazi yao katika jimbo la magharibi la Darfur nchini humo katika kipindi cha mwaka 2003 pekee.

Msudan atakayekwenda Israel anahatari ya kunyongwa pindi atakaporudi nyumbani.

Kwa upande wake Shevy Korzen, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika linaloshughulikia wafanyakazi wahamiaji anasema tatizo kubwa ni kwamba Israel haina utaratibu maalum wa kuongoza shughuli za wakimbizi, hivyo inahitaji kutunga mwongozo wa wazi na kutoa hifadhi inayostahili kwa wakimbizi.

Aidha amesema unapofika wakati wa kuamua nani abaki ama nani arudi alikotoka,uamuzi wa Israel huwa ni wa pupa na kutolea mfano Agusti, 2007 ilirudisha wasudan 48 nchini Misri, waliokuwa wakitafuta hifadhi ya ukimbizi, ambao baadaye 20 kati yao walirudishwa Sudan.

Kwa mara ya kwanza wakimbizi walipoanza kuingia nchini humo miaka michache iliyopita, Israel iliwapa ukazi wa muda wasudan 600 kutoka Darfur, na kuwapa vibali vya kazi Waeritrea 2000.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuwahudumia wakimbizi, Karibu watu elfu 5 na mia tano wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi wamevuka mpaka wa Misri na Israel katika kipindi cha mwaka uliopita pekee.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya nje ya Israel, katika kikao cha baraza la mawaziri, Februari 24, Waziri Mkuu wa Israel alilifananisha wimbi hilo la wakimbizi kama Tsunami na kutaka mawaziri wake kuwafukuza elfu, 4,500 walioingia kinyume cha sheria.

Hata hivyo, hilo halikutokea, badala yake Israel ikaamua kuzingatia madai ya Wasudan na Waeritrea yaliyotolewa na Shirika la Kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa.

Hamed kama watu wengine wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi, alikamatwa na jeshi la Israel na kuwekwa kizuizini katika kambi ya jeshi kwa siku mbili na baadaye kuachiwa huru na kusajiliwa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi mjini Tel Aviv, ambapo kwa sasa anaishi kwa kuhudumiwa na Shirika lisilo la kiserikali kwa kumpa chakula na malazi.

Si Umoja wa Mataifa wala Israel inayotoa chakula, maji wala hifadhi. Bila ya kibali cha kazi, hawezi kufanya kazi kihalali ili kuweza kujihudumia mwenyewe.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW