1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Winchi yaanguka na kuuwa zaidi ya 100 Mecca

12 Septemba 2015

Serikali ya Saudi Arabia inachunguza kuanguka kwa winchi ya ujenzi katika Msikiti Mkuu wa Mecca ambayo imeuwa takriban watu 107 na kuahidi ibada ya hija ya kila mwaka itaendelea kama kawaida.

Winchi ilioanguka katika Msikiti Mkuu katika mji mtakatifu wa Mecca.
Winchi ilioanguka katika Msikiti Mkuu katika mji mtakatifu wa Mecca.Picha: picture-alliance/dpa/AA/O. Bilgin

Takriban watu wengine 200 walijeruhiwa wakati winchi hiyo kubwa ilipouangukia msikiti huo mojawapo ya maeneo matakatifu kabisa ya Waislamu duniani wakati waumini walipokuwa wamekusanyika kwa sala ya Ijumaa.(11.09.2015).

Mamia kwa maelfu ya mahujaji tayari wamewasili Mecca kwa ajili ya ibada ya Hija mojawapo ya tamasha kubwa kabisa la kidini duniani ambalo mwaka jana limevutia mahujaji milioni mbili.

Afisa wa serikali ya Saudi Arabia aliyekataa kutaja jina lake amesema hija ya mwaka huu itaendelea kama kawaida licha ya ajali hiyo iliyotokana na dhoruba ya upepo mkali na mvua.Afisa huyo amekaririwa akisema "Kwa hakika haitoathiri hija ya msimu huu na sehemu ilioathirika yumkini ikarekebishwa katika siku chache zijazo."

Uchunguzi wa ajali kufanyika

Indonesia taifa lenye idadi kubwa ya Waislamu duniani imesema raia wake wawili wameuwawa katika ajali hiyo wakati Malaysia na Iran zimesema raia wao ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa.

Ajali ya kuanguka kwa winchi katika Msikiti Mkuu wa Mecca.Picha: picture-alliance/dpa/AA/O. Bilgin

Wakati viongozi wakitowa rambi rambi zao gavana wa mji wa eneo la Mecca Mwana Mfalme Khaled al- Faisal ameamuru kufanyika uchunguzi kwa tukio hilo.

Abdel Aziz Naqoor ambaye anasema anafanya kazi katika msikiti huo ameliambia shirika la habari AFP kwamba ameliona winchi kubwa la ujenzi likianguka baada ya kupigwa na dhoruba.

Amesema isingelikuwa kwa daraja la Al- Tawaf idadi ya majeruhi na vifo ingekuwa kubwa zaidi,daraja hilo linalozunguka Kaaba takatifu lilikuwa kama kinga ya winchi hilo lililoanguka.

Mamia wajitolea damu

Kaaba jengo kubwa lenye umbo la mraba liko katikati ya msikiti huo ambapo Waislamu duniani huelekea wakati wanapofanya ibada zao.

Waumini wakichukuwa picha kufuatia ajali ya kuanguka kwa winchi katika Msikiti Mkuu wa Mecca.(12.09.2015)Picha: picture-alliance/dpa/AA/O. Bilgin

Mwandishi wa habari mwenyeji nchini Saudi Arabia Kamal Idris ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Wasaudi na wageni walikuwa katika misururu hapo Ijumaa usiku kutowa damu kusaidia manusura wa ajali hiyo.Kwa mujibu mwa mwandishi huyo kulikuwa na watu zaidi ya 100 katika msururu wakisubiri zamu yao kutowa msaada huo wa damu katika mojawapo ya hospitali.

Picha za ajali hiyo kwenye mtandao wa Twitter zimeonyesha miili iliorowa damu imetapakaa sakafuni ambapo sehemu ya juu ya winchi hiyo ambayo inaonekana kupindika au kukatika ilipoangukia jengo lenye ghorofa kadhaa.

Mkanda wa video kwenye mtandao wa YouTube umeonyesha watu wakipiga makelele na kukimbia baada ya kusikika kwa kishindo kikubwa cha kuanguka kwa winchi hiyo.

Dhoruba yasababisha ajali

Mabaki ya winchi hiyo rangi nyekundu na nyeupe yalionekana yakiwa yamelala kwenye sakafu ambayo imechimbika.Kulikuwa na winchi nyengine kadhaa zilizosimamishwa kwenye eneo hilo.

Ajali ya kuanguka kwa winchi katika Msikiti Mkuu wa Mecca.Picha: picture-alliance/dpa/AA/O. Bilgin

Siku za Ijumaa ambapo ni siku ya ibada kuu ya wiki kwa Waislamu Msikiti huo Mkuu kwa kawaida huwa unajaa sana.

Ahmed bin Mohammad al - Mansouri msemaji wa msikiti miwili mikuu mitakatifu amekaririwa na shirika la habari la Saudi Arabia akisema sehemu ya winchi ilianguka saa 11 na dakika 10 jioni " kutokana na upepo mkali na mvua kubwa."Shirika hilo la habari la Saudi Arabia limesema mvua zaidi na upepo mkali unatarajiwa kuendelea Jumamosi.

Kuendelezwa kwa misikiti kwakosolewa

Irfan al-Alawi muasisi mwenza wa Wakfu wa Utafiti wa Turathi ya Kiislamu amelilinganisha janga hilo na lile linalosababishwa na bomu.Amesema kwamba maafisa wa serikali wamezembea kwa kuachia kuwepo kwa winchi kadhaa zikizunguka msikiti huo.

Kuendelezwa kwa Msikiti Mkuu wa Mecca.Picha: picture-alliance/dAP Photo/K. Mohammed

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawajali juu ya turathi na hawajali juu ya afya na usalama.Alawi ni mkosoaji mkubwa wa kuendelezwa upya kwa misikiti hiyo mitakatifu ambapo anasema ni sawa na kufuta uhusiano wa dhahiri mtu anaoweza kuugusa na Mtume Muhammad.

Hii sio mara ya kwanza kwa mahujaji kukumbwa na majanga huko Mecca.Hapo mwaka 2006 mamia ya watu waliuwawa katika mkanyagano wakati wa kumpiga mawe shetani kwenye eneo jirani la Mina ajali kama hiyo ilitokea miaka miwili kabla.

Lakina hija takriban imekuwa haina kabisa ajali katika miaka ya hivi karibuni kwa sababu ya miradi hiyo ya mabilioni ya dola.Kazi imekuwa ikifanyika kutanuwa eneo la Msikiti Mkuu kwa kilomita za mraba 400,000 ili kuwezesha msikiti huo uwaingize watu hadi milioni 2.2 kwa wakati mmoja.

Inaelezwa kwamba takriban mahujaji 800,000 wamewasili kufikia Ijumaa kwa ajili ya ibada ya Hija ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 21 na ambayo kwayo kila Muislamu mwenye uwezo anatakiwa kuitekeleza angalau mara moja katika uhai wake.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Isaac Gamba