WINDHOEK :Rais Mugabe ashtumu IMF
1 Machi 2007Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anashtumu Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF kwa kusababisha umasikini zaidi katika mataifa ya Afrika.Shirika hilo hutoa misaada ya dharura ya fedha kwa mataifa m,asikini. Rais Mugabe aliyasema hayo katika mkutano wa biashara ulioandaliwa na Jumuiya ya Viwanda na Biashara ya Namibia mjini Windhoek.
Nchi ya Zimbabwe imewekewa vikwazo vya misaada na shirika la IMF kwasababu ya kutolipa madeni inayodaiwa.Mfumko wa bei kwa sasa nchini humo unafikia asilimia 1600 kwa mwaka.Wakati huohuo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu walifanya maandamano nje ya ubalozi wa Zimbabwe mjini Windhoek ili kupinga uongozi wa Rais Mugabe.
Waandamanaji hao wanatoa wito kwa Rais Mugabe na serikali yake kuheshimu kazi ya watetezi wa haki za binadamu,kuyapa nafasi mashirika ya habari ya bianafsi vilevile kuruhusu vyama vya upinzani vya kisiasa kushiriki katika masuala ya uongozi.
Rais Mugabe anatoa wito wa ushirikiano zaidi kati ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC.
Makundi ya kutetea haki za binadamu vilevile jamii ya biashara nchini Namibia kwa upande wao wanakashifu ziara hiyo ya Rais Mugabe na kueleza kuwa hilo linatoa ishara mbaya kwa jamii ya kimataifa inayoshtumu vikali uongozi wake.