WINDHOEK: Waherero wakumbuka mauaji ya ukoloni
12 Januari 2004Matangazo
Watu wa kabila la Herero nchini Namibia na wawakilishi wa Ujerumani walishiriki jana katika kumbukumbu ya mwaka wa 100 wa mauaji ya maelfu ya watu hao wakati nchi hiyo ya kusini magharibi mwa Afrika ilipokuwa chini ya ukoloni wa Mjerumani. Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Balozi wa Ujerumani Wolfgang MASSING amekiri kuwa makosa ya historia yaliendeka na kuomba rasmi radhi ya mauaji hayo huku akitoa mwito wa kufunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano usiokuwa na jazba. Waherero wamekuwa wakidai fidia ya mauaji hayo huku serikali mjini Berlin ikishikilia kuwa msaada wake kwa Namibia ni kwa raia wote na sio pekee kwa wale wanaodai kuwa walitendewa maovu wakati wa enzi hiyo ya ukoloni wa Ujerumani. Kumbukumbu hizo zilizofanyika mji wa Okahandja, uliopo kilomita 70 ya Windhoek, zilihudhuriwa na wajumbe 600 wa jamii ya Waherero, ambao ni asilimia 7 ya wakaazi wa Namibia. Serikali ya Namibia iliwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu Kasisi Hendrik WITBOOI. Watafiti wa kihistoria wanadai kuwa Waherero waliokuwa elfu 60 mwaka wa 1904 walisalia elfu 15 mwaka 1907 baada ya wengine kudaiwa kuuliwa katika vita na Wajerumani.