Witkoff na Kushner kukutana na Putin kujadili vita vya Ukrai
2 Desemba 2025
Kulingana na msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, mazungumzo hayo kati ya Putin na Witkoff yatafanyika mchana wa leo.
Afisa mmoja wa ikulu ya White House amesema mkwewe Trump Jared Kushner ataungana na Witkoff katika ziara yake hiyo nchini Urusi.
Putin amesema mara kadhaa kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo ya amani ila iwapo Ukraine itakataa makubaliano, basi vikosi vya Urusi vitasonga mbele na kuyateka maeneo zaidi.
Haya yanafanyika wakati ambapo viongozi wa Ulaya wameonyesha mshikamano na Rais Volodymyr Zelenskiy, baada ya mazungumzo ya Marekani na Ukraine ya kupitia upya pendekezo la amani ambalo awali lilikuwa linaipendelea Urusi.
Zelenskiy ambaye leo atakuwa anakutana na rais wa Ireland na kulihutubia bunge nchini humo, hapo jana alikutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na baada ya kikao chao wakaungana na viongozi wengine wa Ulaya ikiwemo Ujerumani, Italia na Uingereza kwa njia ya simu.