1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kukabiliana na nzige watolewa na UN

11 Februari 2020

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuyasaidia mataifa ya Afrika Mashariki ambayo yanakabiliwa na janga la kubwa la nzige, ukisema hali inaweza kuwa mbaya zaidi endapo hakutakuwa na juhudi za haraka katika kulikabili.

Somalia ruft Notstand aus wegen Heuschreckenplage
Wataalamu wa Somalia wakikabiliana na nzigePicha: picture-alliance/dpa/AP/B. Curtis

Kitengo cha Umoja wa Mataifa chenye kuhusika na ustawi wa kibinaadamu kilicho chini ya ofisi ya katibu mkuu wa umoja huo kimetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuyasaidia mataifa ya Afrika Mashariki ambayo yanakabiliwa na janga la kubwa la nzige, kikisema hali inaweza kuwa mbaya zaidi endapo hakutakuwa na juhudi za haraka katika kulikabili.

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo hicho ambacho pia kinahusika na kukabiliana na majanga ni kwamba takribani watu milioni 13 katika mataifa yalioathiriwa wapo katika kitisho cha kukumbwa na janga kubwa kabisa la njaa. Milioni 10 pekee wapo hasa katika maeneo ambayo kwa sasa yanakabliana na kadhia ya nzige.

Fedha zaidi zinahitajika

Picha: picture-alliance/dpa/AP/B. Curtis

Mark Lowcock ambae ni mratibu wa misaada ya kibinaadamu na dharura wa Umoja wa Mataifa amesema tayari Umoja wa Mataifa umekwishatoa kiasi cha dola milioni 10 kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo. Hata hivyo ameonya kuwa kiasi hicho hakitoshi na kama hakuna jitihada za haraka katika kukabiliana na hali ilivyo sasa ulimwengu utashuhudia tatizo kubwa baadae mwaka huu.

Zaidi anaelezea Mark Lowcock kwa niaba ya Umoja wa Mataifa."Ninatoa wito kwa nchi zinazohusika, jamii ya kimataifa, wafadhili, kuhama na kuchukua hatua na kushiriki sasa. Kuna hatari ya janga. Tuna wajibu wa kulizuia. Tunalo jukumu la kujaribu jambo hilo. Ni vyema kuanza sasa, ama sivyo hatutaweza."

Hadi wakati huu kundi kubwa la nzige limeathiri hali ya upatikanaji chakula katika mataifa ya Kenya, Ethiopia na Somalia. Na kadhia hiyo pia Jumapili iliyopita imeripotiwa Uganda. Kwa mujibu wa Lowcock janga la nzige ni baya zaidi kutokea katika kipindi cha miaka 70 kwa Kenya, miaka 25 kwa Ethiopia na Somalia. Na sababu kubwa inatajwa kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi.

Shirika lenye kushughulikia chakula duniani FAO limeliita janga hili la sasa la nzige kuwa la kiwango cha juu zaidi kutokana na athari zake kutapakaa katika eneo kubwa la Afrika Mashariki. Na hali inaweza kuwa mabaya zaidi na zaidi na kushindikana kudhibitiwa.

Kumbukumbu zinaonesha kumekuwa na aina sita za nzige wa jangwani, wakiwemo wale waliozuka miaka ya 90, na baadae 1987-89. Na mwisho janga kubwa lilizuka katika miaka ya 2003-05.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW