1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa sera ya pamoja Ulaya

23 Agosti 2015

Mawaziri waandamizi katika serikali ya Ujerumani wametowa wito wa kuwepo kwa sera ya pamoja katika Umoja wa Ulaya kukabiliana na mzozo wa wahamiaji na wakimbizi barani humo.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel (kulia) na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani (kushoto) Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel (kulia) na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani (kushoto) Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Wanachama hao wakuu wawili wa chama cha Social Demokratik ambao ni mawaziri katika serikali ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wametowa wito wa kuwepo kwa sera ya kuwapa hifadhi wakimbizi itakayotumika katika nchi zote za Umoja wa Ulaya kama njia ya kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi kuwahi kushuhudiwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeir na Waziri wa Uchumi Sigmar Gabriel wameliwasilisha wazo hilo katika makala iliochapishwa Jumapili na gazeti la "Frankfurter Allgemeine Sontadszeitung" .

Katika makala hiyo ambapo majina yao yamejitokeza kama waandishi wenza mawaziri hao wawili wamesisitiza kwamba kutokana na mzozo ulioko kwenye eneo la jirani yao idadi ya wakimbizi inayoongezeka na wahamiaji wanaowasili hauonekani kumalizika hivi karibuni.

Wameandika kwamba " Sisi wa Ulaya tunawajibika kwa nafsi zetu wenyewe na kwa dunia kutenda haki kutokana na changamoto kubwa inayotokana na watu hao wanaohitaji msaada." Wameongeza kusema kwamba hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Ulaya kwa jumla hazikuwa za kuridhisha.

Sera ya pamoja

Wameendelea kutowa wito wa kuwepo sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya ya kutowa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji na kutaja vipengele kumi vya kuitekeleza.Miongoni mwa dondoo za mpango huo wa vipengele kumi ni wito wa kugawana wakimbizi kwa haki barani Ulaya.

Wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa/G. Licovski

Wakati mawaziri hao wakieleza kwamba kile walichokiandika ni kule kuwa tayari kusiko kifani kwa raia wenzao wengi kuwapokea na kuwasaidia wakimbizi wajumuishwe katika jamii ya Ujerumani,pia wameonya kwamba jambo hilo halitoweza kudumu iwapo wakimbizi wanaomiminika katika kiwango kisicho kifani hawatogawiwa kwa haki miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Pia wametowa wito wa kutolewa kwa msaada wa dharura kwa nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimeathiriwa zaidi na wimbi hilo la wahamiaji kama vile Italia na Ugiriki ambapo ndipo walikoingilia kwanza wakimbizi katika nchi za Umoja wa Ulaya.Kwa kutambuwa shida ambapo serikali za mitaa itakabiliana nazo kushughulikia kile kinachotarajiwa kuwasili kwa wakimbizi 800,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015 ambapo Ujerumani pia ina tajiriba nazo pia wametaka kutolewa kwa masaada wa kifedha wa muda mrefu kusaidia juhudi za serikali hizo.

Nchi salama

Wakigusia wazo ambalo limekuwa likitetewa kwa kiasi kikubwa na wanachama wa chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Demokratik katika wiki za hivi karibuni Steinmeier na Gabriel wametowa wito wa kuwepo orodha ya Umoja wa Ulaya ya "nchi salama walikoingilia kwanza wahamiaji ".

Wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa/G. Licovski

Ujerumani tayari imezitaja nchi kadhaa na yumkini ikaongezea kwenye orodha yake nchi ambazo zinawania kujiunga na Umoja huo wa Ulaya wenye nchi wanachama 28.Mawaziri hao wameona kuna mkanganyiko katika fikra hiyo kwamba nchi katika Balkan ya magharibi zinaweza kustahiki kujiunga na Makubaliano ya Ushirikiano na Umoja wa Ulaya wakati huo huo zikionekana kuwa hazifai kuhesabiwa kama nchi salama kwa watu wanaotafuta hifadhi katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Takriban nusu ya watu waliowasili Ujerumani hadi sasa mwaka huu wakitaka kupwatiwa hadhi ya hifadhi wametokea Balkan ya magharibi na hawana nafasi ya kupewa hifadhi.

Wahamiaji wasiostahiki

Mawaziri hao wameainisha haja ya kuwarudisha haraka wale ambao hawastahiki kupatiwa hifadhi ili fedha hizo zitumike kwa ajili wakimbizi wanaohitaji kweli ulinzi.

Purukushani kati ya polisi na wakimbizi Macedonia.Picha: Reuters/O. Teofilovski

Mwisho Steinmeir na Gabriel wameelezea kwamba njia pekee ya kupambana na tatizo hilo kwa mtizamo wa muda mrefu ni kutafuta njia za kuboresha hali katika nchi ambapo watu wanaona kuwa wanalazimika kukimbia.

Wamemalizia kwa kusema " Kuleta utulivu katika nchi ambazo zinasambaratika, kudhibiti matumizi ya nguvu na mizozo ya kiraia lazima kufanyike sambamba na juhudi za pamoja za kuendeleza uchumi pamoja na kuleta matumaini ya kweli ya kiuchumi na kijamii hususan miongoni mwa vijana katika nchi walikozaliwa."

Mapendekezo yao hayo yanakuja wiki moja baada ya Kansela Angela Merkel kutumia mahojiano yake na kituo cha televisheni cha taifa ZDF kutowa wito wa kuwepo kwa sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji.

Onyo la Italia

Pia Jumapili waziri wa mambo ya nje wa Italia ameonya kwamba mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yanahitaji kutafuta njia bora zaidi ya kuratibu juhudi za kushughulikia mzozo huo kwa kusema kwamba hali hiyo inaweza kutishia uwepo wa uhuru wa mipaka katika kanda ya Shengen ya nchi za umoja huo.

Paolo Gentiloni waziri wa mambo ya nje wa Italia.Picha: picture-alliance/dpa/C. Peri

Paolo Gentiloni ameliambia gazeti la Jumapili la "II Messagero" kwamba kilioko hatarini ni moja ya nguzo muhimu za Umoja wa Ulaya : Nyendo huru za wananchi.

Ameuliza tunaweza kufikiria Umoja wa Ulaya bila ya kuwa na Shengen ?Je turudi katika mipaka yetu ya zamani ? Ameongeza kusema "Wahamiaji hawawasili Ugiriki, Italia au Hungary.Wanawasili barani Ulaya na ndio maana taratibu za kuwapokea inabidi ziwe za aina moja kwa Ulaya nzima ."

Mwandishi : Mohamed Dahman/DW/dpa/AFP

Mhariri :Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW