1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa Umoja Israeli wadhihirisha tofauti kubwa

20 Septemba 2019

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu Benny Gantz wametoa wito wa kuundwa kwa serikali ya muungano kufuatia uchaguzi wa nchi hiyo ambao haujatoa jibu mwafaka.

Israel Netanjahu Rivlin und Gantz
Picha: AFP/Y. Sindel

Hesabu rasmi ya matokeo ya kura hii leo ambayo iko karibu kukamilika imethibitisha mkwamo katika uchaguzi mkuu wa Israeli wiki hii  na kukiweka chama cha Benny Gantz kuwa cha ushindi lakini bila ya fursa ya kuunda serikali ya muungano mkubwa.

Mapendekezo ya wapinzani yaliogubikwa na tofauti nyingi yanaashiria kuwa taifa hilo huenda likakumbwa na kipindi kirefu cha hali isiyoeleweka na wanasiasa wa pande zote wameonya kuhusu uwezekano wa kuandaliwa kwa uchaguzi wa tatu katika muda usiozidi mwaka mmoja tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa. Katika taarifa aliyotoa kupitia video, Netanyahu amesema hakuna chaguo lingine ila kuunda serikali ya muungano mkubwa na kwamba hawawezi na hakuna sababu ya kuandaa uchaguzi wa tatu. Baada ya kushindwa kuunda muungano baada ya uchaguzi wa mwezi Aprili, Netanyahu aliitisha uchaguzi wa Jumanne na badala yake kushuhudia mkwamo mwingine wa kisiasa.

Huku kura zote zikiwa zimehesabiwa kufikia jana, chama cha Buluu na Nyeupe kinachoongozwa na Gantz kilipata viti 33 vya bunge kati ya viti 120. Chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kilijipatia viti 31. Hakuna chama kinachoweza kufikia wingi wa kura wa viti 61 hata baada ya kuungana na vyama vidogo ambavyo ni washirika wao.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu asalimiana na mpinzani wake mkuu Benny Gantz wakati wa ibada ya ukumbusho ya aliyekuwa rais wa Israel Shimon Peres.Picha: AFP/G. Cohen-Magen

Chama cha pekee kinachoweza kuleta tofauti ni kile cha Yisrael Beitenu kinachoongozwa na Avigdor Lieberman kilichojipatia viti vinane ambapo Lieberman amekataa kushirikiana na upande wowote na badala yake kutaka serikali ya muungano mkubwa na vyama hivyo viwili vikuu. Pendekezo la Netanyahu limekatiliwa na Gantz ambaye chama chake cha Buluu na Nyeupe kimesema kuwa kitashauriana tu na chama cha Likud iwapo Netanyahu atajiondoa katika kinyang'anyiro kukabiliana na masaibu yake ya kisheria.

Netanyahu anatarajiwa kushtakiwa kutokana na misururu ya kesi za ufisadi katika miezi ijayo. Hata hivyo wabunge wa chama cha Likud bado ni waaminifu kwa Netanyahu na hawajatoa ishara yoyote ya kutaka kumng'atua. Akiongea na wanahabari, Gantz amesema kama chama kikubwa, anapaswa kuongoza serikali ijayo. Gantz aliyekuwa mkuu wa jeshi la nchi hiyo ameongeza kuwa watu walichagua umoja na kwamba wanaitaka Israeli kupewa kipaumbele kushinda jambo lolote na hivyo basi chama chake chini ya uongozi wake kilishinda katika uchaguzi.

Rais wa Israel, Reuven Rivlin ametangaza kuwa ataanza mashauriano na vyama vyote siku ya Jumapili kuamua anayepaswa kuunda serikali ijayo. Uchaguzi wa Jumanne uliadhimisha mara ya kwanza kwa Israel kuandaa uchaguzi mara mbili katika muda wa mwaka mmoja.