Wito watolewa Afrika kupewa viti vya kudumu katika UN
27 Septemba 2018Viongozi wa Afrika wanaohudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York wameendelea kutoa miito ya kukuza ushirikiano, ambapo Rais Hage G. Geinob wa Namibia amesema ana hofu anapoona dunia ikigawika zaidi, huku Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akikiambia kikao hicho kuwa imani kwa serikali inazidi kupungua kadiri habari kuhusu ufisadi zinavyotangazwa katika vyombo vya habari na kwenye na mitandao ya kijamii.
Akihutubia viongozi katika kikao hicho kikuu cha Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Kenyatta amesema katika miongo ya hivi karibuni, Afrika imepoteza mamilioni ya dola kwa njia haramu za kuhamishiwa nchi za nje huku akionya kuwa kinachofanywa barani humo kinapaswa kufanyiwa sehemu nyingine za ulimwengu, akiulaumu vikali ule alioutaja kuwa ufisadi katika mfumo wa kifedha na kisheria ulimwenguni.
Kenyatta: Afrika ipewe viti vya kudumu
Kando ya hilo, rais huyo wa Kenya amegusia haja ya bara la Afrika kuwa na nafasi za kudumu kwenye vyombo vikuu vya maamuzi vya Umoja wa Mataifa, akisema kuwa bara hilo linastahiki:
"Kenya inaungana na wengine kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu vyenye haki na majukumu sawa na wengine ikiwemo haki ya kura ya turufu, pamoja na viti vingine zaidi ambavyo si vya kudumu jinsi tunavyojua. Afrika haijawakilishwa vya kutosha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatujawakilishwa kabisa katika kiwango cha kudumu. Ukosefu huu wa haki wa kihistoria ni ishara wazi ya mfumo wenye mapendeleo unaochangia upungufu w akutoaminiana kati ya mataifa."
Naye nyota wa zamani wa kandanda wa kimataifa aliye sasa rais wa Liberia, George Weah, alihutubia kikao hicho kwa mara ya kwanza na kusema matatizo ya uongozi ni mengi.
Weah alikiambia kikao hicho kuwa Liberia itaanza misururu ya mazungumzo ya amani, ili wasirudie makosa ya kale yaliyowasababishia hasara.
Mnangagwa: Vikwazo dhidi ya Zimbabwe viondolewe bila masharti
Hali ilikuwa tofauti mwaka huu kuhusu hotuba ya rais wa Zimbabwe. Tofauti na rais wa zamani, Robert Mugabe, aliyekuwa mshambulizi mkali dhidi ya nchi za Magharibi, rais mpya Emmerson Mnangagwa alionekana kutaka kuwa mwanachama anayewajibika katika Umoja huo.
Huku akitaka kuvutia wawekezaji ili kuinua uchumi ambao umeporomoka, Mnangagwa alitoa wito wa kutaka vikwazo ambavyo alivitaja kuwa vimeendelea kuwepo kinyume na sheria, kuondolewa bila masharti:
Mnangagwa alisisitiza haja ya amani, umoja na kuvumiliana huku akisisitiza kuwa nchi yake imefungua milango kwa biashara.
Rais Hage Geinob wa Namibia amesema ameingiwa hofu na hatua ya ulimwengu kuendelea kugawika zaidi na kuelekea kufanya maamuzi ya kibinafsi. Amesema hayo yanaenda kinyume na misingi ya demokrasia.
Nana Akufo Addo: Kuna haja ya Afrika kujiendeleza bila kutegemea misaada
Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana ametetea uwekezaji mkubwa unaofanywa na China barani Afrika, akisema ni bayana kuwa njia za maendeleo ambazo bara hilo lilikuwa likizifuata kwa miongo mingi hazifanyi kazi na ndio maana sasa linajaribu njia nyingine.
Rais Akufo-Addo amewasilisha kile alichokitaja kuwa mpango wa kuwepo Afrika inayojiendeleza bila ya kutegemea misaada, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuelewa na kuunga mkono.
Kikao hicho kimeingia siku yake ya tatu leo, ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania, Augustine Mahiga, anatarajiwa kuhutibia kikao hicho kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli ambaye hakuhudhuria.
Mhariri: Mohammed Khelef