1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito watolewa kwa EU Kongeza msaada Afghanistan

16 Septemba 2021

Mashirika 24 yanayohusika na masuala ya haki za binadamu na wakimbizi yametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuongeza msaada wake kwa watu wanaojaribu kuikimbia Afghanistan.

Pictures of the Week in the Middle East Photo Gallery
Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Katika taarifa, mashirika hayo yanayozijumuisha Amnesty International, Caritas Europa, Kamati ya Uokoaji ya Kimataifa, Oxfam na Shirika la msalaba mwekundu, yamesema kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kugawanya majukumu badala ya kukwepa uwajibikaji kwa waomba hifadhi hao na kuwapa ulinzi. Mashirika hayo yameonya kuwa watu milioni 18 wanahitaji kwa dharura msaaada wa kibinadamu nchini Afghanistan hii ikiwa karibu nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo.

Katika takwimu mpya zilizotolewa Alhamisi, Ofisi inayowashughulikia waomba hifadhi barani Ulaya EASO imeripoti kuwa idadi ya waomba hifadhi katika Umoja wa Ulaya iliongezeka kwa asilimia 20 mnamo mwezi Julai hata kabla ya Taliban kuchukuwa madaraka Afghanistan. EASO imesema kuwa maombi ya kutafuta hifadhi ya  raia wa Afghanistan yalifika 7,300 mwezi Julai hata kabla ya taifa hilo kuanguka mikononi mwa kundi la Taliban hili likiwa ongezeko la asilimia 21 zaidi ya ilivyokuwa mwezi Juni na la muda wa miezi mitano mfululizo. Takriban waomba hifadhi 1200 walikuwa watoto ambao hawakuandamana na mtu.

Rais wa Afghanistan wasubiri kutoa pesa zao benki mjini KabulPicha: Bernat Armangue/AP/picture alliance

Kupitia taarifa, Ofisi hiyo ya EASO imesema  kwa jumla, watu elfu 50 walituma maombi ya kutaka ulinzi kote katika mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na mataifa ya Norway na Uswisi yasiokuwa wanachama, hii ikiwa idadi kubwa zaidi katika muda wa mwezi mmoja tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona na kwamba idadi hiyo ilikaribiana na idadi ya maombi ya kutafuta hifadhi ya raia wa Syria. Pengo la kuomba hifadhi kati ya raia wa Afghanistan na Syria limekuwa likipungua kwa haraka tangu Desemba mwaka 2020.

Umoja wa Ulaya umeahidi kuongeza msaada wa kibinadamu nchini Afghanistan na kutoa usaidizi kwa mataifa jirani kuyawezesha kuwapokea wakimbizi wapya.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan Sheikh Rashid Ahmed, leo amemuambia Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi anayezuru nchini humo kwamba  hakuna wakimbizi wapya kutoka Afghanistan walioingia nchini humo tangu kundi la Taliban lilipochukua uongozi wa taifa hilo jirani mwezi uliopita. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Ahmed alisema, Pakistan ilituma malori ya msaada wa chakula nchini Afghanistan kujaribu kuepusha mzozo wa kibinadamu nchini humo. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Grandi amelishukuru taifa hilo kwa kuwahudumia wakimbizi milioni 3 kutoka Afghanistan katika miongo ya hivi karibuni.

 

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW