Wito watolewa kwa Israel na Palestina
18 Machi 2014Aidha, Rais Obama amewataka viongozi wa nchi hizo mbili kufanya maamuzi magumu ya kisiasa ili mazungumzo hayo yaweze kusonga mbele.
Akizungumza na Abbas katika Ikulu ya Marekani, Rais Obama amezitaka Palestina na Israel kukubaliana kuhusu mfumo wa kuendelea na mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yanayosimamiwa na Marekani, ambayo muda wake utakamilika Aprili 29, mwaka huu.
Abbas ambaye amekwenda nchini Marekani wiki mbili baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa muda unapita huku mazungumzo hayo yakisuasua na kuitaka Israel kuwaachia huru wafungwa wa Palestina ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, ili kuonyesha kuwa wako tayari na makini kwa juhudi za amani ya Mashariki ya Kati.
Abbas alikaa pembeni ya Rais Obama, katika kiti kilichokaliwa wiki mbili zilizopita na Netanyahu, ambaye alilalamika kuwa Israel imetekeleza mipango yake kama sehemu ya mazungumzo hayo ya amani, huku Palestina ikiwa haijatekeleza kwa upande wake.
Rais Obama amesema kuwa makubaliano hayo yanapaswa kuzingatia misingi ya mipaka ya taifa la Palestina iliyowekwa miaka 47 iliyopita.
Abbas apuuzia madai ya Israel
Akipuuza madai ya Israel kutaka itambuliwe kuwa taifa la Wayahudi, Abbas alimkumbusha Rais Obama kuwa Wapalestina wamekubali uhalali wa Israel tangu mwaka 1988 na kwamba mwaka 1993 walilitambua taifa la Israel.
Baada ya kukutana na Rais Obama, Abbas pia alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ambapo pamoja na mambo mengine walibadilishana mawazo kuhusu uwezekano wa kusonga mbele mazungumzo hayo.
Kwa upande mwingine mpatanishi Mkuu wa Palestina katika mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, Saeb Erekat, amesema Israel lazima ichague kati ya kujenga makaazi ya Walowezi katika Ukingo wa Magharibi na makubaliano ya amani, lakini haiwezi kufanya mambo yote hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu, Erekat amesema kuwa makubaliano yoyote lazima yahusishe eneo la mipaka lililochorwa la taifa la Palestina, lililowekwa mwaka 1967, kabla Israel haijalitwaa kimabavu eneo la Ukingo wa Magharibi, Gaza na Jerusalem Mashariki.
Hata hivyo, Erekat ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Abbas, amethibitisha kuhusu msimamo wake kwa Rais Obama, wa kukataa kuitambua Israel kama taifa la Wayahudi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir