1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito watolewa wa mashauriano kati ya Algeria na Morocco

26 Agosti 2021

Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Jumuiya ya Kiarabu and Saudi Arabia zimetoa wito wa mashauriano ya kutatua mvutano kati ya Algeria na Morocco. Siku ya Jumanne, Algeria ilitangaza kuvunja uhusiano wake na Morocco.

Algerien kappt Beziehungen zu Marokko
Picha: Fateh Guidoum/AP/picture alliance

Taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya kigeni ya Saudi Arabia imesema kuwa taifa hilo limetoa wito kwa mataifa hayo mawili ya Algeria na Morocco kutoa kipaombele katika juhudi za kuafikia usalama na uthabiti.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu Ahmed Aboul Gheit pia ameyahimiza mataifa hayo kudumisha utulivu na kuepusha kuongezeka kwa mvutano huo. Libya ambayo inapakana na Algeria inasema kuwa inasikitishwa na kudorora kwa uhusiano kati ya mataifa hayo ya Algeria na Morocco na pia kutoa wito wa utulivu. Pia imetaka kufanywe mazungumzo ya kikanda pembezoni mwa mkutano ujao wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, uliopangwa kufanyika Septemba 7 hadi 9 huko Cairo.

Siku ya  jumanne  Algeria ilisema kuwa inavunja rasmi uhusiano wake na Morocco kwa mujibu wa taarifa ya waziri wa mambo ya nje  Ramtane Lamamra kutokana na kurefushwa kwa vurugu ambazo zaidi zinahusu eneo la Magharibi mwa Sahara.

Saad-Eddine El Othmani- Waziri mkuu wa MoroccoPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Lamamra alisema kuwa hali ya sasa na ya baadaye ya Algeria inahujumiwa na matendo ya Morocco na kwa hivyo jibu hilo la umma na rasmi la Algeria kuhusu mienendo ya uhasama ya Morocco linaonesha haja ya ombi la haraka la busara ya kimantiki badala ya kubashiri mabaya ambapo kwa bahati mbaya kunaonekana kuwa chanzo cha misimamo ya Ufalme wa Maghreb kuelekea Algeria. Lamamra ameongeza kuwa katika hali zote Algeria inakataa kukubaliana na mienendo isiyostahili inayoishtumu vikali.

Wizara ya mambo ya nje ya Morocco imesema kuwa taifa hilo linasikitishwa na uamuzi ulioutaja kuwa usiofaa wa Algeria wa kuvunja uhusiano huo wa kidiplomasia na kutaja baadhi ya sababu zilizotolewa na Algeria kuwa zisizokuwa na maana. Kupitia taarifa, wizara hiyo imeongeza kuwa hatua hiyo ilitarajiwa kwa kuzingatia ongezeko la mvutano katika wiki za hivi karibuni.

Kwa muda mrefu, Algeria imekuwa na msuguano na Morocco hasa kuhusiana na eneo la Magharibi mwa Sahara, lililokuwa koloni la Uhispania ambalo Morocco linalitazama kama sehemu muhimu ya ngome yake lakini pia ambapo Algeria imeliunga mkono vuguvugu la uhuru la Polsario. Ushindani wao ulichukuwa mwelekeo mpya mwaka jana wakati aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alipotambua eneo hilo kuwa chini ya mamlaka ya Morocco kwa kubadilishana na Morocco kurudisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel..

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW