1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wizara 12 zachukuliwa na vyama vya upinzani Afrika Kusini

Hawa Bihoga
1 Julai 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza Baraza lake jipya la Mawaziri siku ya Jumatatu, na kutenga wizara 12 kwa vyama vya upinzani, huku wizara nyeti ikiwemo Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje zikisalia kwa ANC.

Afrika Kusini | Cyril Ramaphosa na John Steenhuisen
Rais Cyril Ramaphosa akimsabahi Kiongozi wa chama cha upinzani DA John Steenhuisen.Picha: South African GCIS/AP/picture alliance

Chama Kiukuu cha Upinzani nchini humo cha Demokratic Alliance DA, kitachukua viti sita, huku kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen akitangazwa kuongoza wizara ya kilimo.

Chama tawala cha ANC kimechukua wizara 20, ikiwa ni pamoja na wizara nyeti kama vile Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Nishati na Fedha.

Baraza hilo ambalo lina wizara 32, linatajwa kuwa ni kubwa zaidi likiwa na ongezeko la wizara mbili, ikilinganishwa na miaka iliopita.

Soma pia:Rais Ramaphosa hatimaye ateua baraza jipya la mawaziri

Akihutubia katika televisheni ya taifa Ramaphosa amesema serikali mpya ya mseto imejizatiti katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa Waafrika Kusini.

"Katika siku hii tumeunganisha nguvu zetu kwa pamoja, Tumeungana kama Waafrika Kusini, tukiwa na matumaini makubwa." Alimesema Rais Ramaphosa.

Aliongeza kwamba "tuchukue tumaini hili, ili kila mmoja wetu aweze kuunganisha nguvu katika kuijenga Afrika Kusini ya ndoto yetu."

Vipaumbele vya serikali mpya ya Afrika Kusini

Serikali hii mpya ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo la kusini mwa Afrika, imeundwa na vyama 11, inatarajiwa kuongoza taifa hilo ambalo linauchumi imara zaidi barani humo.

Raia wa Afrika Kusini akipeperusha bendera ya taifa hilo wakati wa sherehe za kuapishwa kwa Rais Cyril RamaphosaPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Chama cha ANC cha Ramaphosa kilipoteza wingi wa viti kwenye Bunge kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, katika uchaguzi wa Mei 29 na kupoteza hadhi ya kuongoza serikali peke yake.

Serikali hii mpya inayojumuisha vyama vya upinzani imepanga kutoa kipaumbele katika masuala kadhaa muhimu, ikiwemo ukuaji wa uchumi, haki za kijamii kadhalika kustawisha demokrasia ya nchi.

Soma pia:Chama cha MK chajiunga na muungano wa upinzani Afrika Kusini

Kupambana na umaskini, ukosefu wa ajira, na uhalifu pia ni miongoni mwa vipaumbele, pamoja na kushughulikia rushwa na unyonyaji wa serikali ambao umekuwa ukilalamikiwa na wakaazi wa taifa hilo.

Ikumbukwe kwamba muungano huo wa uongozi umeundwa bila makubaliano yoyote ya muungano thabiti. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wametilia shaka uthabiti na ufanisi wa aina hiyo ya serikali.

Taifa la Afrika Kusini limezidi kuwa muhimu katika medani za kimataifa kutokana na nafasi yake ya kijografia kwenye bara la Afrika, ambalo ni tajiri kwa malighafi zinazohitajika kuelekea matumizi ya nishati safi.

Taifa hilo pia ni mwanachama pekee kutoka barani Afrika katika kundi la mataifa  20 yaliyostawi na yanazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani G20.

Ramaphosa aapishwa Afrika Kusini

00:59

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW