Wolfgang Schaueble spika mpya Bundestag
24 Oktoba 2017Wakati huo huo chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD kimeapa kwamba enzi mpya imewadia nchini Ujerumani wakati kikishiriki kwa mara ya kwanza kikao cha bunge jipya , ambapo kimeweza kuonesha ubavu wake.
Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Wolfgang Schaeuble alichaguliwa kuwa spika wa bunge kwa kupata kura 501 kati ya kura 705 zilizopigwa na wabunge wenzake kwa ajili ya wadhifa huo wa bunge la taifa , Bundestag.
"Bwana Mwenyekiti nimekubali matokeo ya uchaguzi."
Wolfgangn Schäuble ametilia mkazo umuhimu wa watu kuheshimiana bungeni,akisemam unabidi uwe mfano kwa jamii. Mnamo miezi iliyopita kauli za kuvunjiana hishma na kudharauliana zimekuwa zikisikika. Kauli kama hizo hazina nafsi katika bunge atakaloliongoza amesema Schaeuble.
Chama cha Alternative for Germany , chama mbadala kwa Ujerumani , AfD , ambacho kilifanikiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwezi uliopita, mara moja kilionesha kwamba kitaleta changamoto kubwa bungeni hapo baadaye.
Hoja ya kwanza bungeni
Kikionesha kwamba kutakuwa na mivutano zaidi bungeni katika miaka minne ijayo chama cha AfD kilikuwa cha kwanza kuwasilisha hoja bungeni kupinga mabadiliko katika sheria za bunge ambazo zinazuwia mmoja kati ya wabunge wake kutoa hotuba ya ufunguzi katika bunge hilo.
Wakati hoja hiyo ilishindwa mara moja na wabunge wengine wote, mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha AfD bungeni Bernd Baumann alifananisha hali hiyo na hatua ya Hermann Goering wakati wa enzi za Wanazi mwaka 1933 alipomzuwia kiongozi wa kikomunist Clara Zetkin kutoa hotuba ya ufunguzi katika kikao cha bunge.
Matamshi hayo yalipokelewa kwa mshangao mkubwa wa wabunge na kushutumiwa na mbunge wa chama cha Free Democrats FDP Marco Bueschmann kuwa, hayakuwa na mashiko.
Lakini mashambuliaji hayo yanaonekana kama mwanzo wa mivutano mikali katika vikao vijavyo, wakati wabunge waandamizi katika chama cha AfD wamekuwa mara kwa mara wakivunja utaratibu kwa kutoa madai ya uasili wa Ujerumani na kutoa changamoto kwa utamaduni wa Ujerumani wa kujihisi na makosa kuhusiana na vita vikuu vya pili vya dunia pamoja na mauaji ya wayahudi ya Holocaust.
Baumann amesema , Bunge la zamani limemaliza muda wake. wananchi wameamua , enzi mpya inaanza sasa." Kuanzia sasa , masuala yatajadiliwa upya, sio mbinu zenu na ujanja mnaofanya bungeni lakini masuala kama sarafu ya euro, deni kubwa, idadi kubwa wa wahamiaji, mipaka iliyo wazi na uhalifu mkubwa katika mitaa ya miji yetu, ameongeza Baumann.
Mpambano mwingine unafukuta leo wakati wabunge watakapochagua makamu wa spika. Kila chama kina haki ya kumteua makamu wake katika bunge, lakini yeyote awaye anapaswa kupigiwa kura bungeni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman