1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfowitz kufanya ziara Afrika mwezi huu

Lillian Urio8 Juni 2005

Rais mpya wa Benki ya Dunia, Paul Wolfowitz, mwezi huu atatembelea nchi nne barani Afrika. Anataka kushuhudia mwenyewe mahitaji ya kimaendeleo ya bara hilo.

Paul Wolfowitz, Rais mpya wa Benki ya Dunia
Paul Wolfowitz, Rais mpya wa Benki ya DuniaPicha: AP

Akiongea na waandishi wa habari, kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa Benki ya Dunia, Bwana Wolfowitz amesema atalipa bara la Afrika kipaumbele.

Watu wengi wamekuwa wakisubiri kwa hamu Bwana Wolfowitz aanze kazi. Wakijadili kama atafanya kazi ya kuendeleza siasa za Marekani. Jambo ambalo waliokuwa wakimpinga walisema litatokea. Lakini matarajio yao hayajatokea.

Kwani, Bwana Wolfowitz anaelekea kuwa mstari wa mbele kwa kuendeleza ajenda za aliye mtangulia, rais wa zamani wa Benki ya Dunia, James Wolfensohn.

Katika mkutano na waandishi wa habari Bwana Wolfowitz alisema:

“Nitalipa bara la Afrika kipaumbele. Pia Benki ya Dunia inalipa kipaumbele. Nadhani Benki hii ina nafasi ya aina pekee barani Afrika na bara hilo lina mahitaji ya kipekee.”

Rais huyo mpya wa Benki ya Dunia anajua kwamba kusini mwa Afrika bado watu milioni 300 kila siku wanaishi kwa matumizi ya chini ya dola moja, ya kimarekani. Ameeleza kwamba mwezi huu atatembelea Burkina Faso, Nigeria, Rwanda na Afrika Kusini, iliaone mwenyewe mahitaji tofauti katika nchi hizi.

Lakini Bwana Wolfowitz hategemei kukutana na viongozi wa nchi tu amesema:

“Nategemea kukutana na viongozi muhimu wa nchi hizo zote. Pia nitatembelea miradi, nitakutana na watu maskini, ambao ndio walengwa wa kazi za Benki hii. Nataka kuonana na mashirika ya kiraia, haswa yale yanayowakilisha wanawake. Nadhani kwamba kuwawezesha wanawake kushiriki kwenye masuala ya maendeleo ni muhimu katika kupata mafanikio.”

Kabla ya kuanza ziara yake ya Afrika, Bwana Wolfowitz atakutana na mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa G8, mjini London. Moja ya suala litakalojadiliwa ni mpango mpya wa misaada ya kifedha kwa ajili ya kuongeza miradi ya kuleta maendeleo.

Suala hili pia litakuwa ajenda kuu katika mkutano wa G8, utakaofanyika Scottland mwezi wa Julai.

Bwana Wolfowitz hajatoa mapendekezo yoyote kuhusu suala hili na pia hajaonyesha kwamba tayari analo suluhisho. Lakini ameungana na wale wanao toa wito wa kuwepo na ongezeko la rasilimali, akielezea:

“Ni muhimu sana kwa njia yoyote ile, kuongeza rasilimali ili kuiwezesha Afrika iwe na nafasi ya kubadilika.”

Bwana Wolfowitz amesisitiza kwamba ni muhimu Afrika ichangie kwa kiasi kikubwa kwa kutumia nguvu yake yenyewe. Kwa mfano kwa kupambana na ufisadi. Hamna haja ya kujenga barabara mpya wakati, wakati hakuna bidhaa zitakazo zitumia.

Siri ya mafanikio ya kupambana na umaskini ni kuchanganya, uwezeshaji wa kufanya biashara, uwekezaji binafsi na msaada wa kiuchumi wa kitaifa.

Mwaka uliopita Benki ya Dunia ilikuwa na miradi 334 barani Afrika na iliyogarimu milioni 16.6, dola za Kimarekani. Katika suala la kuipa Afrika mikopo ya kifedha, benki ya Dunia inaongoza duniani kote.
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW