1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
KandandaUjerumani

Wolfsburg yamsaini kiungo wa Denmark Christian Eriksen

11 Septemba 2025

Klabu ya Wolfsburg imetangaza kumsajili kiungo Christian Eriksen kwa uhamisho huru. Usajili huo unamfanya Eriksen kuwa mchezaji wa kwanza wa Denmark kujiunga na VfL Wolfsburg katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Euro 2024 | Denmark | Christian Eriksen
Kiungo wa kati wa timu ya taifa ya Denmark Christian EriksenPicha: Sven Hoppe/picture-alliance

Klabu ya VfL Wolfsburg imemsajili kiungo wa Denmark Christian Eriksen kwa uhamisho huru, klabu hiyo ya Bundesliga ilitangaza mnamo Jumatano 11.09.2025.

"Wolfsburg ni klabu yangu ya kwanza katika ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga – ninasubiri kwa shauku kubwa safari hii mpya. Ninaamini tunaweza kufanikisha jambo kubwa pamoja hapa Wolfsburg," amesema Eriksen.

Eriksen amejiunga leo na kikosi cha kwanza katika mazoezi ya timu na amepongezwa na kocha Paul Simonis.

"Leo amekamilisha mazoezi yake ya kwanza. Kesho tutakuwa tena uwanjani. Kisha tutaangalia kama atafanikiwa kujumuishwa kwenye mechi ya Jumamosi. Lakini mazoezi yake ya kwanza yalikuwa mazuri." 

Wolfsburg wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mechi ya Bundesliga dhidi ya Köln siku ya Jumamosi, lakini kocha tayari ameeleza kwamba Eriksen hatakuwepo kwenye sehemu ya kikosi cha kwanza.

"Lakini huenda akawa sehemu ya wachezaji watakaokuwa kwenye benchi," ameongeza.

Eriksen, mwenye umri wa miaka 33, amesaini mkataba wa kuichezea klabu hiyo hadi mwaka 2027. Kiungo huyo alikuwa bila klabu tangu mkataba wake na Manchester United ulipomalizika mwezi Januari, na alikuwa akifanya mazoezi katika klabu ya Malmö nchini Uswidi.

Kompany aongoza mazoezi ya Bayern Munich kwa mara ya kwanza

01:56

This browser does not support the video element.

"Tunafurahia sana fursa hii iliyojitokeza kwa muda mfupi. Kupitia Christian Eriksen, tunapata mchezaji mwenye uzoefu mkubwa. Ubora wake uwanjani na haiba yake ni sifa zitakazokuwa na msaada mkubwa kwa wachezaji wetu vijana," alisema mkurugenzi wa michezo wa Wolfsburg, Sebastian Schindzielorz.

Eriksen alipata mshtuko wa moyo wakati wa mashindano ya Ulaya ya EURO mwaka 2021 kabla ya kufanyiwa huduma ya dharura ya moyo na kurudishwa katika hali ya kawaida kwa kutumia kifaa cha "defibrillator."

Tukio hilo lilitokea dakika ya 42 ya mchezo dhidi ya Finland na lilisimamisha mechi kwa muda huku wachezaji na mashabiki wakiwa katika hali ya mshangao na huzuni. Baadaye, Eriksen alipelekwa hospitali akiwa imara na alirejea uwanjani miezi kadhaa baadaye akiwa amewekewa kifaa cha kufuatilia mapigo ya moyo (ICD).

Baada ya kupona, alijiunga na klabu ya Brentford kabla ya kuhamia Manchester United mwaka 2022.

Hata hivyo kiungo huyo hakujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Denmark kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.