1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yashuka Bundesliga baada ya miaka 29

26 Mei 2026

Wolfsburg imeshushwa Bundesliga baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Paderborn kwenye muda wa nyongeza, huku Crystal Palace ikisaka taji la kwanza la Ulaya chini ya Oliver Glasner.

Bundesliga 2025/26 | VfL Wolfsburg vs. SC Paderborn 07
VfL Wolfsburg yashushwa daraja baada ya miaka 29 katika ligi kuu ya Ujerumani.Picha: Swen Pförtner/dpa/picture alliance

Klabu ya Soka ya Wolfsburg imeshushwa daraja kutoka Bundesliga baada ya kupoteza 2–1 ugenini dhidi ya Paderborn katika mechi ya marudiano iliyochezwa hadi muda wa nyongeza. Wolfsburg imekuwa ikicheza ligi kuu ya Ujerumani bila kukosa tangu ilipopandishwa daraja mwaka 1997.

Baada ya miaka 29 bila ya kushushwa daraja, Wolfsburg walipata pigo chini ya Paderborn, Licha ya kutangulia kufunga kupitia Dzenan Pejcinovic dakika ya 2 ya mchezo,  mambo yalianza kuwaendea mrama kunako dakika ya 13 wakati beki Joakim Maehle alipoonyeshwa kadi nyekundu.

Dakika saba kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza, Paderborn walisawazisha kupitia Filip Bilbija, na mechi ilikamilika kwa sare ya moja moja na kuingia katika muda wa ziada.

Laurin Curda dakika 10 baada ya kuanza muda wa nyongeza aliliipa Paderborn nafasi ya kupanda Bundesliga kwa mara ya tatu katika historia yao.

Baada ya kusawazisha, Paderborn walikosa nafasi kadhaa za wazi, huku kipa wa Wolfsburg Kamil Grabara akiokoa mara nyingi.

Wolfsburg, ambao waliwahi kuwa mabingwa wa ligi mwaka 2009 na washindi wa Kombe la Ujerumani mwaka 2015, waliepuka shoka la kushuka daraja kwenye mechi za mchujo za mwaka 2017 na 2018. Huku safari mara mbili za awali za Paderborn kwenye Bundesliga zote zilimalizika kwa kushuka daraja.

Palace yatafuta kombe la Ulaya

Kocha wa Crystal Palace Oliver Glasner anataka kufunga ukurasa wake wa miaka miwili kwa "mwisho mkamilifu” kwa kushinda dhidi ya Rayo Vallecano kwenye fainali ya Uropa Conference League mjini Leipzig leo Jumanne.

Oliver Glasner akisherehekea kombe la FA kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 120 ya Crystal Palace.Picha: Kirsty Wigglesworth/AP/picture alliance

Mwaustria huyo ataiongoza Palace kwa mara ya mwisho baada ya kipindi cha mafanikio makubwa tangu ajiunge mwaka 2024. Aliletea klabu hiyo kombe lao la kwanza katika historia ya miaka 120 kwa kutwaa Kombe la FA kwenye msimu wake wa kwanza. Msimu huu alianza kwa kuifunga Liverpool kwenye Community Shield, na sasa ana nafasi ya kuipa Palace taji lao la kwanza la Ulaya.

Rayo walimaliza La Liga pointi moja nyuma ya Getafe, lakini sasa wanaweza kuwazidi majirani zao kwa kufuzu Europa League kwa mara ya pili katika historia yao. Wamefika fainali baada ya kuwaondoa Strasbourg, Palace walipoteza 2–1 dhidi ya Wafaransa hao kwenye hatua ya makundi.

Hata hivyo akiwa ameiongoza Frankfurt kutwaa taji la Europa League mwaka 2022 na kufika fainali ya Kombe la Ujerumani mwaka uliofuata, Glasner anaonekana kuwa uzoefu zaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW