1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yatoka sare na Leverkusen

3 Aprili 2017

Mario Gomez alifunga mabao matatu ndani ya dakika saba wakati Wolfsburg ilitoka sare ya mabao 3-3 na Bayer Leverkusen. Katika mechi nyingine, Ingolstadt iliifunga Mainz 2-1

Deutschland Bayer Leverkusen gegen VfL Wolfsburg | Mario Gomez
Picha: picture alliance/dpa/M. Meissner

Mshambuliaji huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 31 sasa amefunga mabao sita katika mechi take nne za mwisho katika Bundesliga. Huyu hapa mfungaji huyo wa Hat trick Mario Gomez "N vizuri sana kwamba kulikuwa na mabao mengi kuliko moja. Kunabaadhi ya mechi zilizopita amb apo sikuwa na utulivu kuanzia mwanzo na leo tulikuwa nyuma mabao mawili kwa sifuri. Ni kutokana na hali hiyo ambapo nilikuwa mtulivu zaidi na makini zaidi kwenye mechi. Na nna furaha kwa mabao hayo. Lakini inanikera sana kuwa hatukuweza kushinda mechi hii".

Matokeo hayo yameiacha Wolfsburg, mabingwa wa Ujerumani mwaka wa 2009, wakiwa pointi moja tu juu ya nafasi za kushushwa ngazi wakati Leverkusen ikiwa juu yao na pengo la pointi mbili tu.

Lewandowski alifunga hat trick yake ya tatu msimu huuPicha: Reuters/M. Dalder

Awali, Ingostadt walirejesha matumaini ya kuepuka shoka la kushushwa ngazi baada ya kuilaza Mainz 2-1. Ingolstadt ni wa pili kutoka nafasi ya mkia, pointi saba kati yao na nambari sita Augsburg.

Kichapo hicho kimewatumbukiza tena Mainz katika vita vya kushushwa ngazi maana wako nafasi ya 14 na wako juu ya timu tatu za mkia kwa tofauti ya mabao pekee. Hadergjonaj ni winga wa ingoldast ambaye alifunga bao moja katika ushindi huo "Tumekuwa na bahati leo: mara nyingi tumekuwa na bahati mbaya kwa kushindwa kutumia vyema nafasi za kufunga mabao. Tulifahamu kuwa utakuwa mchuano mkali dhidi ya mpinzani ambaye yuko katika nafasi ya chini na sasa lazima tuendelee kupambana kama tulivyofanya leo"

Katika upande wa juu wa msimamo wa ligi, Bayern Munich walisalia kileleni na pengo la pointi 13 baada ya kuwakandika Augsburg 6-0. Katika mechi hiyo, Robert Lewandowski alifunga hat trick yake ya tatu katika Bundesliga msimu huu. Msikilize Lewandowski "Nadhani kama timu nzima tumeonyesha kuwa tunataka kuendeleza mchezo wetu mzuri - iwe ni Bundesliga au Champions League - na leo tumefurahia sana mchezo".

Mpoland huyo sasa ana mabao 24 katika ligi msimu huu, sawa na Pierre-Emerick Aubameyang aliyeifungia Borussia Dortmund katika sare yao ya 1-1 na Schalke katika derby ya Bonde la Ruhr

Aubameyang alifunga bao lake la 24 katika Bundesliga msimu huuPicha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

Nambari mbili RB Leipzig ilirejea kwa kishindo kufuatia vichapo vya mfululizo kwa kuwacharaza washika mkia Darmstadt 4-0. Ralph Hasenhüttl ni kocha wa Leipzig "Ni muhimu kuwa tumeshinda tena leo katika uwanja wa nyumbani baada ya mechi mbili mfululizo bila ushindi. Tuliona katika kipindi cha kwanza kuwa hatukucheza vyema. Nibaada ya kufunga mabao 2-0 ambapo tuliweza kujikomboa na hilo lilikuwa muhimu".

Kinyang'anyiro cha Bundesliga kitaendelea tena katikati ya wiki hii ambapo hapo kesho, nambari tatu kwenye ligi Hoffenheim itajaribu kuwawekea breki Bayern Munich na kusoea karibu na kandanda la Champions League msimu ujao. Werder Bremen watawaalika Schalke

Wakati nambari sita Cologne watacheza dhidi ya nambari saba Eintracht Frankfurt. Dortmund wataangushana na SV Hamburg, wakati Jumatano Leipzig watakuwa wageni wa Mainz. Katika mechi nyingine za Jumatano, Wolfsburg itacheza dhidi ya Freiburg, Augsburg itaikaribisha Ingolstadt, na washika mkia Darmstadt watawaalika Bayer Leverkusen. Borussia Moenchengladbach, iliyoko nafasi ya kumi, itacheza dhidi ya Hertha

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga