1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTaiwan

Waziri aitahadharisha Taiwan kuhusu uvamizi wa China

6 Machi 2023

Waziri wa Ulinzi wa Taiwan Chiu Kuo-Cheng, ametowa tahadhari hii leo kwamba kisiwa hicho kinapaswa kuwa tayari mwaka huu kwa uvamizi wa ghafla wa jeshi la China katika maeneo yaliyoko karibu na ardhi yake.

Tamko hilo limetolewa kufuatia ongezeko la mivutano ya kijeshi katika eneo tete la rasi ya Taiwan. China imeongeza shughuli zake za kijeshi katika maeneo yanayoizunguka Taiwan katika miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo bado Taiwan haijaripoti tukio lolote la wanajeshi wa China kuingia kwenye ardhi yake, japo utawala wa kisiwa hicho umeapa kutekeleza haki yake ya kujilinda na kurudisha mashambulio itakapovamiwa.

Akijibu maswali ya wabunge bungeni, Chiu alisema Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) huenda likapata visingizio vya kuingia katika maeneo ya karibu na eneo la anga na bahari ya Taiwan wakati kisiwa hicho kikiongeza mabadilishano yake ya kijeshi na Marekani, hatua iliyoikasirisha Beijing.