Wosia wa mwisho wa Maalim Seif Sharif
19 Februari 2021Taarifa za kuumwa Maalim Seif zilitangazwa na Naibu katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, Nassor Mazrui wakati akitibiwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na baadae kusafirishwa jijini Dar es Salaam kupatiwa matibabu zaidi ambapo kuugua kwake kulichukua takriban siku 18 hadi kukatisha uhai wake.
Soma pia: Maalim Seif azikwa Pemba
Wakati Maalim Seif akiwa mgonjwa akipatiwa matibabu alizungumza na viongozi wake akiwemo Nassor Ahmed Mazrui na kuwapa wosia huku akiwasisitizia juu ya kuendeleza umoja ndani ya chama chake pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe alizungumza mbele ya Rais wa Zanzibar, Dokta Hussein Ali Mwinyi muda mfupi baada ya kumaliza taratibu zote za mazishi yake na kumueleza namna ambavyo Maalim Seif alimpa kauli yake ya mwisho ambayo kwake ni sawa na kuagana.
Kwa sasa Maalim Seif hayupo tena dunia suala la wananchi ni nani atakayevaa kiatu chake cha kuendeleza yale mazuri aliyopapigania kwa miaka zaidi ya 30, lakini faraja walionayo wananchi wengi ni kuyaelekeza matumaini yao kwa Rais Mwinyi ambaye tayari ameshaahidi mara kadhaa kuyaendeleza Maridhiano ya Kisiasa ya kuwaunganisha Wazanzibari wote.