1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wa kiafrika mjini Wuhan wahofia mambukizi

Zainab Aziz Mhariri: Yusuf Saumu
5 Februari 2020

Mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona unawaweka waafrika walioko kwenye jimbo la Wuhan nchini China katika hali ya sintofahamu. Wanataka kurejeshwa nyumbani lakini wanachokitaka Waafrika hao hakiwezekani!

Äthiopien Flughafen Addis Abeba | Sicherheitsmaßnahmen gegen Coronavirus
Picha: Getty Images/L. Dray

Wanafunzi waafrika wapatao 5000 wako nchini China wakiwa na matumaini ya kurudishwa nyumbani ili kuepuka hatari ya virusi vya Corona. Hata hivyo zoezi hilo huenda likashindikana kwa waafrika wengi. Mpaka sasa ni Morocco tu iliyoweza kuwaondoa watu wake kutoka Wuhan mahala palipolipuka maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais wa Senegal Macky Sall alitangaza hapo jana mjini Dakar kwamba Senegal haitawarudisha wanafunzi wake nyumbani. Sawa na nchi nyingine za Afrika Senegal pia haina uwezo wa kuwarudisha wanafunzi wake kwa sababu haina miundombinu stahili, haina wahudumu wenye uzoefu na wala haina vifaa vya karantine. Rais wa Senegal amesema nchi yake itatoa msaada wa fedha kwa wanafunzi wake walioko Wuhan lakini siyo jambo rahisi kuwarudisha nyumbani.

Hali ni ngumu kwa wanafunzi wa waafrika katika jimbo la Wuhan kwa sababu shughuli  takriban zote zimefungwa ikiwa pamoja na mabenki. Mwanafunzi mmoja kutoka Guinea amesema ni vigumu kupata fedha kutokana na mabenki kufungwaAmeeleza kuwa akiba ndogo ya chakula waliyonayo inakaribia kumalizika lakini ubalozi wa Guinea umewataka wanafunzi wa nchi hiyo wavute subira.

Mwanafunzi kutoka Ethiopia pia amelalamika juu ya hali inayowakabili. Ameiambia DW  kwamba hawaruhusiwi kutoka nje, amesema kwa sasa hawana matatizo ya afya, lakini anauliza ni kwa muda gani wataweza kuvumilia hali ya kufungiwa ndani?

Rais wa Senegal Macky SallPicha: Imago/Xinhua/Lv Shuai

Barani Afrika kwenyewe hakuna watu walioambukizwa virusi vya Corona.Taarifa za hapo awali juu ya maambukizi hayo nchini Ivory Coast, Kenya na Ethiopia hazikuthibishwa na shirika la afya duniani WHO.

Hata hivyo shirika la habari la utangazaji la Uingereza BBC limeripoti kwamba mwanafunzi  mmoja kutoka Cameroon ameambukizwa katika jimbo la Wuhan. Wakati huo huo mashirika ya ndege ya nchi kadhaa za Afrika yamesimamisha safari za kwenda China. Shirika pekee la ndege linaloendelea kufanya safari za kwenda China ni la Ethiopia.

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amefananisha mlipuko wa virusi vya corona na mlipuko wa homa ya Ebola katika Jamhuri ya kidemkrasia ya Kongo amesema milipuko hiyo imeonyesha jinsi ilivyo muhimu kujitayarisha badala ya kueneza taharuki.

Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba kutokana na juhudi za kimataifa maambukizi ya virusi vya Ebola yaliweza kupungua na kwamba kutengenezwa kwa chanjo ni ushindi mkubwa.

Bwana Gebreyesus amesema licha ya nchi nyingi za Afrika kuweza kujifunza kutokana na mlipuko wa Ebola na kuweza kuweka  mifumo ya tahadhari, mifumo ya afya ya nchi hizo nyingi bado ni dhaifu.

Chanzo:/Herrmann, Clarissa (HA Afrika)

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW